KOMBE LA DUNIA QATAR: Meli, boti zaandaliwa kwaajili ya mashabiki

MAMBO yamezidi kunoga kuelekea michuano ya Kombe la Dunia itayofanyika Qatar, Novemba mwaka huu. Unaambiwa meli kubwa zaidi ya 17 za kisasa zimeandaliwa kwa ajili ya mashabiki ambao wataishi humo hadi michuano hiyo itakapomalizika. Huu ni mwendelezo wa uchambuzi wa mambo yanayoendelea Qatar kabla ya michuano hiyo kuanza kurindima.


Meli 17 zimendaliwa Qatar

Meli kubwa 17 za kisasasa zimeandaliwa kwa ajili ya mashabiki ambao wataishi humo ikielezwa ndani ya meli hizo kuna vyumba vingi na huduma mbalimbali zitakazotolewa kipindi chote wakati michuano ya Kombe la Dunia ikiendelea nchini Qatar.

Baada ya kuthibitishwa rasmi kila meli moja itabeba mashabiki 40,000. Meli hizo zitakuwa na sehemu ya chakula, vinywaji na malazi mwanzo mwisho bila ya kuboreka wakati michuano ikiendelea.

Imeelezwa mashabiki 12,000 watakaa katika meli yenye vyumba 6,000 ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya mashabiki kuelekea michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika kwa mara kwanza katika nchi ya falme za Kiarabu.

Pia, kuna hoteli zilizoandaliwa kwa ajili ya mashabiki watakaopenda. Kila hoteli moja ina jumla ya vyumba 60,000 ambavyo zimelipiwa. Unaambiwa vyumba vya hoteli vimejaa kutokana na wingi wa mashabiki watakaosafiri kwenda Qatar.

Mmiliki wa hoteli ya Katara Hospitality, Hamad Abdulla al-Mulla anasema Qatar imeandaa hoteli zenye vyumba 60,000 kwa ajili ya mashabiki watakaoingia Qatar kushabikia mataifa yao.

“Qatar imeandaa hoteli ambazo zipo tayari kwa ajili ya mashabiki. Mbali na hoteli hizo vilevile kutakuwa na meli zenye vyumba muda wote michuano itapokuwa ikiendelea. Idadi ya vyumba vya meli kila moja itakuwa ni vingi,” alisema bosi huyo.

Mbali na huduma za hoteli na meli, Qatar imeandaa mahema mengi kwa ajili ya mashabiki ambayo yatapatikana katika maeneo mbalimbali ya jangwani karibu kabisa na viwanja vya mpira ili wasipate ugumu wa kufika kushuhudia kipute wakati kinapigwa.

Mashabiki zaidi ya milioni 1.5 wanatarajia kusafiri kwenda Qatar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia, na kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa wataanza kumiminika kabla ya michuano kuanza ili kuepuka msomangamano na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza baada ya kuanza kwa mashindano.

Vilevile Qatar imerekibisha miundombinu ya mfumo wa usafirishaji, kwani safari za kwenda viwanjani kuangalia mechi zitachukua dakika 35, hivyo mashabiki hawatapata karaha hususan kwenye ishu za usafiri. Mfumo huo utawasaidia kuangalia mechi zaidi ya mbili kwa siku moja.


Boti zitakuwepo

Imethibitishwa pia kwamba familia za mastaa wa soka ambao watashiriki michuano ya Kombe la Dunia wamendaliwa boti maalumu za kifahari na wataishi humo hadi ikatakapomalizika.

Kwa mujibu wa ripoti familia za wachezaji wa timu ya taifa England watafikia kwenye boti ya kifahari iliyoandaliwa kwa ajili yao na vilevile huduma zitakazotolewa ndani ya boti ni pamoja na vinywaji mbalimbali ikiwamo pombe kali bila ya kuvunja sheria.

Kwa mujibu wa Daily Mail mastaa kama Harry Kane, Jordan Henderson na Raheem Sterling walibariki mpango huo kutokana na usalama wa familia zao kipindi chote watakachokuwepo nchini Qatar.

Vyumba vitakavyokuwa ndani ya boti hizo vitakuwa vya kifahari kuendana na mahitaji ya familia hizo.

Boti na meli hizo zitakuwepo karibu kabisa na Jiji la Doha ili kuwapa nafasi wanafamilia kushangilia ushindi pamoja na ndugu zao ambao ni wachezaji.

Hata hivyo, zipo pia taarifa kwamba timu ya taifa ya England huenda ikafikia katika hoteli ya kifahari ya Souq Al-Wakra iliyopo jijini Doha kuendana na masuala ya kiusalama.