KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Zali la mentali

DOHA, QATAR. HAIZIDI miezi miwili siku zilizobaki kabla ya pazia la fainali za Kombe la Dunia 2022 kufunguliwa rasmi huko Qatar.

Na sasa makocha wa timu za taifa wanakuna vichwa watokeje kwenye uteuzi wa wachezaji watakaounda vikosi vyao kwenye fainali hizo zitakazofanyika kwa mara ya kwanza Mashariki ya Kati.

Kwenye machaguo ya vikosi, makocha wakati mwingine wamekuwa wakiteua vikosi na kuwajumuisha wachezaji ambao wanakwenda nao kwenye fainali mbalimbali na hawawatumii hata kwenye mechi moja.

Kwa mfano, kocha Gareth Southgate wakati wa fainali za Euro 2020 aliwateua mastaa Ben Chilwell na Conor Coady kwenye kikosi na hawakutumika mechi yoyote.

Kutokana na hilo, hawa hapa mastaa ambao waliwahi kutajwa kwenye vikosi vya nchi kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia, ambapo walishinda mechi za ubingwa bila ya kucheza mechi yoyote.


Franco Baresi

Franco Baresi aliichezea Italia mechi 81 kwenye soka la kimataifa, lakini zote hizo zilikuja baada ya kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia 1982. Kipindi hicho, beki Baresi alikuwa na umri wa miaka 22 na alikuwa sehemu ya kikosi cha Azzurri kwenye fainali zilizofanyika Hispania. Wakati Enzo Bearzot akiwashtua vigogo waliokuwa wakipewa nafasi ya kubeba ubingwa wa fainali hizo, mastaa wake Paolo Rossi na Marco Tardelli walikuwa gumzo kubwa. Lakini, aliyekuwa gumzo zaidi ni Baresi - ambaye alishinda medali ya ubingwa wa Kombe la Dunia bila ya kucheza mechi yoyote kwenye fainali hizo na hakuwa amechezea timu ya wakubwa.


Angelo Peruzzi

Miaka 24 baadaye, Italia ilibeba tena ubingwa wa dunia. Safari hii ni Peruzzi - ambaye mechi yake ya kwanza Azzurri alicheza mwaka mmoja baada ya Baresi kuacha kuichezea timu hiyo mwaka 1995 - naye alisherehekea kushinda medali ya ushindi ya Kombe la Dunia bila ya kucheza mechi yoyote kwenye fainali hizo. Kipa huyo wa Juventus alitamba na Bianconeri katika miaka ya tisini na alikuwa Namba Moja wa Italia kwenye Euro 96. Miaka 10 baada ya michuano hiyo, soka lake lilielekea ukingoni, lakini aliitwa kwenye kikosi cha Marcello Lippi kilichokwenda kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia 2006 huko Ujerumani kilipoichapa Ufaransa kwa mikwaju ya penalti. Peruzzi alipewa medali bila ya kucheza mechi yoyote.


Raul Albiol

Beki wa Hispania, Raul Albiol anaweza kujiona ni mtu mwenye mkosi linapokuja suala la soka la kimataifa, lakini anaweza kujihesabu pia ni mwenye bahati. Beki huyo wa kati alikuwa sehemu ya kikosi cha La Roja kilichobeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2010 na Euro 2012, lakini hakucheza dakika yoyote kwenye michuano yote hiyo miwili. Albiol ameitumikia Hispania kwenye mechi 58 kwa kipindi kinachozidi muongo mmoja, ambapo mara yake ya kwanza ilikuwa 2007 na mwisho ilikuwa 2021. Hata hivyo, hajawahi kuwa na kuonja raha ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwenye mwaka ambao taifa lake liliibuka na ubingwa. Awamu yake moja aliyocheza mechi ya Kombe la Dunia ilikuwa 2014 huko Brazil kwenye mechi dhidi ya Australia, ambapo Hispania haikuwa na maajabu yoyote.


Erik Durm

Ukizungumzia Kombe la Dunia 2014, Ujerumani ilikuwa na kikosi matata kwelikweli. Mastaa kibao wa maana waliitwa na kocha Joachim Low, huku wengine wakiwamo mfungaji wa bao la nusu fainali, Andre Schurrle - naye ameshajiuzulu soka la kimataifa. Lakini, Erik Durm aliteuliwa kwenye kikosi hicho akiwa ametimiza miaka 22, alikuwa mmoja wa wachezaji vijana kabisa katika kikosi hicho ambapo alikuwa akiibukia kutoka kwenye kikosi cha Borussia Dortmund. Hata hivyo, kwenye fainali hizo za Brazil, Durm hakucheza mechi yoyote na hivyo kushinda medali ya ubingwa akiwa hajacheza mechi na baada ya hapo, ameitumikia Ujerumani mara saba.


Alphonse Areola

Kutokana na Hugo Lloris kuwa nahodha wa Ufaransa iliyobeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2018 huko Russia, nafasi ya makipa wengine kupata nafasi ya kucheza ilikuwa finyu sana. Kipa Steve Mandanda alipewa nafasi ya kucheza kwenye mechi ya sare ya bila kufungana dhidi ya Denmark iliyokuwa ya kukamilisha hatua ya makundi kwa sababu Les Bleus tayari ilikuwa imeshafuzu hatua ya 16, lakini kwa Areola hakupata nafasi yoyote ya kucheza. Akiwa na umri wa miaka 25 wakati huo, Areola alikuwa anatokea kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain kilichoshinda mataji matatu ndani ya msimu mmoja, lakini alishindwa kupata nafasi kucheza kwenye kikosi cha Ufaransa iliyoshinda ubingwa Russia.


Adil Rami

Areola hakuwa pekee kwenye kikosi cha Ufaransa, ambaye hakucheza mechi hata moja kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia. Adil Rami, ambaye alikosa kidogo tu kuwamo kwenye kikosi cha Les Bleus kilichokwenda Kombe la Dunia 2010, alipata nafasi ya kuwapo kwenye kikosi cha Ufaransa kilichokwenda kwenye fainali hizo miaka minane baadaye. Akiwa na umri wa miaka 32 wakati fainali hizo za Kombe la Dunia 2018, Rami alicheza mechi za kirafiki za kujiandaa na michuano hiyo dhidi ya Ireland na Italia, lakini huko Russia aliishia tu kukaa benchi, Raphael Varane na Samuel Umtiti wakianza mbele yake. Lakini, mwisho wa fainali hizo alishinda medali ya ubingwa akiwa hajacheza mechi yoyote.