KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Messi kidogo aikose safari ya Qatar

DOHA, QATAR. TANGU wiki iliyopita ligi mbalimbali duniani kote zimesimama ili kupisha mechi za kimataifa za kirafiki zinazotambuliwa na Shirikisho la kimataifa la Vyama vya Soka Duniani (Fifa).

Mechi hizi ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya zile timu zilizofuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar ambazo zinatarajiwa kufunguliwa Novemba 20.

Mechi hizi unaweza ukadhani ni za lele mama lakini kumbe wachezaji wanakamiana kiasi cha kuchezewa tafu mbaya zisizo za kimchezo.

Katika mechi iliyochezwa nchini Argentina kati ya wenyeji dhidi ya Honduras Jumamosi ilishuhudia Staa na Mchezaji Bora wa Dunia mara Saba, Lionel Messi akichezewa rafu mbaya dakika ya 39.

Katika mchezo huo ambapo Argentina ilishinda mabao 3-0 na mshambuliaji wake na nahodha Messi alitupia mabao mawili na alikumbwa vibaya na kuguswa na kiwiko maeneo ya mdomoni.

Rafu hiyo iliyofanywa na kiungo mkabaji, Deybi Flores ambaye alienda kwa kasi kutaka kumpora mpira Messi aliyekuwa ameumiliki mpira huo. Tukio hilo liliamsha hasira kwa wachezaji wa Argentina dhidi ya kiungo huyo.

Wakati Messi akigalala chini wenzake walimvaa kwa ghadhabu Flores kiasi cha kutokea mtafaruku kwa dakika kadhaa. Refa alitumia muda mwingi kuwatuliza na hatimaye alitoa kadi ya njano kwa mchezaji huyo wa Honduras.

Ilikuwa chupuchupu kwa Messi kwani kama kiwiko hicho kingetua vyema mdomini angeliweza hata kujeruhiwa katika eneo la kinywa na meno yaani mdomoni.

Katika kuelekea katika Kombe la Dunia nchini Qatar hakuna mchezaji yeyote ambaye angelipenda apate majeraha kizembe kwani kila mmoja ana kiu ya kutimiza ndoto za kucheza fainali hizo.

Ndio maana tukio hilo liliamsha hasira kwa wenzake mara baada ya kuona rafu hiyo haikua ya kimchezo na ingeliweza kumleta madhara nahodha wao.

Lakini hayo hayamkuti Messi pekee bali hata washambuliaji wengine ikiwamo Cristiano Ronaldo, Kylian Mbappe, Mohamed Salah, Neymar ambao wiki iliyopita na wiki hii timu zao za taifa zimecheza mechi kadhaa za kirafiki.

Pamoja na hekaheka zote wanazopitia bado wanasoka hawa wanaendelea kushiriki michezo hiyo ya kirafiki.

Lakini pia wanasoka hawa wanafanya mambo mengi ambayo yanasaidia sana kuifanya miili yao kuweza kuepuka majeraha hasa yale ya tishu laini.


MAJERAHA YANATOKEA HIVI

Sahau kuhusu umri Ronaldo au Messi ambapo wiki iliyopita nilielezea uhusiano wa majeraha na umri, wachezaji kama hawa wana mbinu kadhaa wanazofundishwa na benchi la ufundi na wataalamu wa afya.

Ikumbukwe ni vigumu kushiriki michezo bila ya kukumbana na majeraha lakini ni vizuri kufahamu mbinu za kupunguza majeraha ya tishu laini ikiwamo misuli, maungio na ligamenti.

Majeraha ya michezo yanaweza kuwa madogo, ya kati na makubwa na huanishwa katika makundi makuu mawili kuendana na aina ya tishu iliyojeruhiwa.

Kundi la kwanza ni majeraha tishu ngumu yaani mifupa ikiwamo kuvunjika na kuteguka au kuhama kwa mfupa katika pango la ungio lake.

Kundi la pili ni majeraha ya tishu laini ambayo aina ya kwanza kitabibu hujulikana kama Strain ambayo ni majeraha ya vijinyuzinyuzi vinavyounda misuli na miishilio ya misuli ijulikanayo kama tendoni.

Aina ya pili ya majeraha ya tishu laini hujulikana kama sprain ambayo yanajitokeza katika nyuzi za ligamenti ambazo hujeruhiwa kwa kuvutika kupita kiwango chake, kuchanika au kukatika pande mbili.

Majeraha ya vijinyuzinyuzi vya misuli hutokea kutokana na kuvutika kupita kiasi au kuchanika, wakati tendoni za misuli zinaweza kukatika au kufyatuka kutoka katika mfupa uliojipachika.

Kazi ya ligamenti ni kuunganisha mfupa na mfupa katika ungio wakati tendoni ni kuunganisha msuli na mfupa na vijinyuzinyuzi vya misuli kazi yake ni kuleta mjongeo kwa kujivuta na kukunjuka.

Wakati wa kucheza yapo matukio yanayoweza kusababisha tishu laini kutanuka kupita kiasi au kutumika sana kupita uwezo wake hivyo kusababisha majeraha.

Kwa kawaida tishu hizi zinaweza kuvutika na kurudi katika hali yake ya kawaida, ila pale mtanuko unapozidi ukomo ndipo hali ya majeraha hujitokeza ikiwamo kuchanika.

Vilevile tishu laini hujeruhiwa kutokana na kutumika huku zikiwa na majeraha ya ndani kwa ndani, hivyo kadiri zinavyotumika ndivyo majeraha yanavyozidi kuwa makubwa.


MBINU ZA KUJIKINGA NI KAMA HIZI

Nyenzo ya msingi ya kupunguza majeraha haya ni kuhakikisha mwili unapashwa moto kabla ya kuingia katika mazoezi au mechi ili kuandaa mwili kwa ajili ya matendo ya michezo kwa ufanisi.

Kupasha moto kunasababisha damu nyingi kutiririka kwa wingi katika misuli hivyo kuifanya misuli kupokea virutubisho muhimu kwa ajili ya utendaji wa seli hivyo kuvifanya viungo kuwa imara kiutendaji.

Wanaepuka kuingia ghafla uwanjani na kucheza au kufanya zoezi bila kupasha kwani mtu aliyetulia viungo vya mwili wake inakuwa haijajiandaa kufanya hivyo matendo hayo.

Wanapasha sana angalau muda wa saa moja kabla ya mechi ngumu au zoezi gumu na wanafanya mazoezi ya kawaida wanahitaji kupasha angalau dakika 5-10.

Wanafanya usingaji (massage) kabla na baada ya mechi au mazoezi kwani husaidia kulainisha misuli na mishipa ya damu kufunguka na kutiririsha damu kwa wingi hivyo kuondoa uchovu.

Wanatumia virutubisho vya protini kabla ya kuingia au kuanza michezo migumu husaidia kupunguza majeraha ya misuli kwani protini ni moja ya kitu muhimu kwa misuli kufanya kazi.

Kumbuka kuwa uwepo wa uchovu na protini kidogo katika misuli husababisha misuli kukakamaa, hivyo kusababisha kupata majeraha kirahisi.


CHUKUA HII

Ukiachana na huduma za timu zao wachezaji mastaa wa kimataifa hujiongeza kwa kuajiri wataalamu wa afya binafsi ikiwamo madaktari, wataalam wa lishe za wana michezo, wafanya masaji na wataalamu wa mazoezi ya viungo.

Hii ni moja kati ya siri kubwa za kufanikiwa kuepukana na majeraha ya michezo hatimaye kudumu na kucheza bila kupata majeraha kwa muda mrefu huku pia wakiwa wanachezeshwa mechi nyingi.

Kushiriki michezo mingi pia ni tiba mojawapo kubwa ya kujikinga na majeraha kwa mchezaji.