Kombe la Dunia 2022: Mmoja hapa anachukua!

DOHA, QATAR. NANI atabeba Kiatu cha Dhahabu cha fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar mwaka huu?

Tuzo hiyo matata kabisa ya Kiatu cha Dhahabu hutolewa kwa mchezaji aliyefunga mabao mengine kwenye fainali hizo.

Mchakamchaka wa fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar umeshavuka hatua ya 16 bora na sasa miamba inajiandaa kuchuana kwenye hatua ya robo fainali. Wakati wachezaji wakiwa kwenye vita ya kusaidia timu zao kubeba ubingwa, purukushani ni kubwa pia kwenye kusaka tuzo ya Kitu cha Dhahabu ili kuondoka Qatar kibabe zaidi.

Utaratibu ni kwamba tuzo ya Kiatu cha Dhahabu inatolewa kwa mchezaji aliyefunga mabao mengi kuliko wengine na kama ikitokea kuna wachezaji wamelingana kwa mabao, basi zinachukuliwa takwimu za kuhusu asisti walizotoa wachezaji hao ili kumpata mmoja aliyehusika kwenye mabao mengi na kukabidhiwa tuzo yake.

Na kama mabao ya kufunga pamoja na asisti zikilingana, basi mshindi wa Kiatu cha Dhahabu atapewa yule aliyecheza dakika chache zaidi na kupata namba hizo zinazostahili kukabidhiwa tuzo hiyo.

Nahodha wa England, straika Harry Kane ndiye aliyenyakua Kiatu cha Dhahabu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018, ambapo alifunga mabao sita wakati kikosi chake cha Three Lions kilipokomea hatua ya nusu fainali.

Kwenye fainali hizo, Kane amefunga bao moja tu hadi sasa jambo linalomfanya kukabiliwa na wakati mgumu katika kutetea tuzo hiyo, huku kukiwa na wakali wengine kadhaa waliowasha moto kwenye kufunga na kujiweka pazuri kubeba tuzo.


Kylian Mbappe - mabao 5, asisti 2

Supastaa wa Ufaransa, Kylian Mbappe amekuwa kwenye kiwango bora kabisa katika fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar kutokana na namna anavyowasha moto. Staa huyo akiitumikia Ufaransa, ambao wanapambana kutetea ubingwa wao waliobeba miaka minne iliyopita huko Russia, ameshafunga mabao matano na kuasisti mara mbili katika dakika 297 alizocheza katika mechi nne za michuano hiyo ya fainali za Kombe la Dunia 2022.


Alvaro Morata - mabao 3, asisti moja

Usiku wa jana Jumanne, straika Alvaro Morata alikuwa na kibarua kizito cha kuivusha Hispania mbele ya Morocco kwenye mchezo wa mtoano wa hatua ya 16 bora. Chochote ambacho Morata atakuwa amefanya katika mechi hiyo kwa maana ya kufunga au kuasisti, basi atakuwa amejiongezea kitu kwenye mchakamchaka wa kuwania tuzo ya Kiatu cha Dhahabu, ambapo kabla ya hapo alikuwa amefunga mabao matatu na kuasisti mara moja katika dakika 126 alizocheza kwenye mechi tatu.


Lionel Messi - mabao 3, asisti moja

Supastaa, Lionel Messi amecheza dakika zote 90 katika mechi nne ilizocheza Argentina kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar hadi sasa. Wakati chama hilo la Amerika Kusini likitinga robo fainali ya michuano hiyo ya Qatar, Messi amehusika kwenye dakika 360, akifunga mabao matatu na kuasisti mara moja. Huduma yake imekuwa kitu muhimu kwenye kikosi cha Argentina, ambacho ni moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa huo wa dunia mwaka huu.


Marcus Rashford - mabao 3, asisti 0

Kwenye kipute cha hatua ya 16 bora kati ya England na Senegal, staa Marcus Rashford alianzia benchi na hivyo kushindwa kuendeleza moto wake wa kufunga mabao kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar kama alivyoanza kwenye hatua ya makundi. Fowadi huyo hadi sasa ameshafunga mabao matatu katika dakika 132 alizocheza kwenye mechi tatu. Rashford bado hajaasisti, huku England yake ikitinga robo fainali ambapo wana mtihani mzito mbele yao dhidi ya Ufaransa.


Bukayo Saka - mabao 3, asisti 0

Winga matata wa mpira, Bukayo Saka ametumika kwenye dakika 214 katika fainali hizo za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar akiwa ndani ya uzi wa England, ambayo kwa sasa imetinga robo fainali wakikabiliwa na mtihani mbele Ufaransa. Hata hivyo, Three Lions inajivunia kuwa na huduma ya Saka, ambaye hadi sasa amefunga mabao matatu katika mechi tatu alizotumikia kikosi hicho kinachojaribu kusaka ubingwa wake wa kwanza wa dunia tangu mwaka 1966.


Cody Gakpo - mabao 3, asisti 0

Uholanzi imetinga hatua ya robo fainali kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar na mtihani unaowakabili mbele yao ni kumenyana na Argentina ya supastaa Lionel Messi. Ni mechi ngumu, lakini jeuri ya Uholanzi ni uwepo wa huduma ya mshambuliaji Cody Gakpo kwenye kikosi chao, ambapo mkali huyo hadi sasa ameshafunga mabao matatu katika dakika 343 alizocheza katika mechi nne za michuano hiyo. Gakpo ameonyesha kiwango bora kabisa huko Qatar akiwa na The Oronje.


Olivier Giroud - mabao 3, asisti 0

Straika Olivier Giroud amefunga bao lake la 52 akiwa na kikosi cha Ufaransa na kuzidi kujiweka pazuri kwenye rekodi yake ya kuwa mfungaji bora wa nyakati zote wa Les Bleus. Chama lake limetinga robo fainali kwenye michuano ya Kombe la Dunia 2022 huko Qatar na mtihani unaowakabili mbele yao ni kukipiga na England. Kwenye fainali hizo za Qatar, Giroud hadi sasa amecheza dakika 227 katika mechi tatu na kufunga mabao matatu yanayomweka kwenye mchakato wa kusaka tuzo ya mabao.


Bruno Fernandes - mabao 2, asisti 2

Kiungo fundi wa mpira, Bruno Fernandes usiku wa jana Jumanne alikuwa na majukumu mazito ya kuivusha Ureno kwenye hatua ya 16 bora ya fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar kwa kukipiga na Uswisi. Kilichotokea kimetokea, lakini kabla ya mechi hiyo, Fernandes alikuwa ameliweka jina lake mahali pazuri kwenye mbio za kusaka Kiatu cha Dhahabu baada ya kufunga mabao mawili na kuasisti mara mbili katika dakika 180 alizokuwa amecheza kwenye mechi mbili.


Wachezaji wengine

Kwenye orodha ya wafungaji wenye mabao mengi kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar inawahusu pia walifunga mara mbili, ambao ni pamoja na Cho Gue-sung wa Korea Kusini kwenye dakika 196, Andrej Kramaric wa Croatia dakika 208, Ferran Torres wa Hispania dakika 144, Breel Embolo wa Uswisi dakika 238, Julian Alvarez wa Argentina katika dakika 208 na Richarlison wa Brazil amefunga mara mbili kwenye dakika 152 kabla ya mechi ya usiku wa juzi Jumatatu.