Klabu 12 zaanzisha Ligi mpya Ulaya, zazua mijadala

Muktasari:

  • Klabu zilizotangaza kuasisi mpango huo zinatoka Italia, Hispania na England, zikiwemo Manchester United, Arsenal na Liverpool.

LONDON, ENGLAND. Klabu 12 kubwa zimetangaza kuanzisha michuano mipya ya soka ya Super League ya Ulaya zikiahidi kuendelea kushiriki ligi za nchi zao, hatua ambayo imepondwa na klabu, vyama vya soka vya nchi na cha wanasoka.
Hatua hiyo inaashiria uwezekano wa mabadiliko makubwa katika uendeshaji wa soka barani Ulaya, lakini walio nyuma ya mpango huo wanatuhumiwa kwa ubinafsi.
Klabu sita zinazoshiriki Ligi Kuu ya England-- Liverpool, Manchester United, Arsenal, Chelsea, Manchester City na Tottenham -- zimo katika mpango huo, pamoja na Real Madrid, Barcelona, Atletico Madrid, Juventus, Inter Milan na AC Milan.
Super League ya Ulaya (ESLP) ilisema waasisi wa michuano hiyo, ambao ni klabu 12, wamekubaliana kuanzisha "mashindano ya katikati ya wiki" lakini wataendelea "kushiriki michuano ya taifa ya nchi zao".
Ilisema inategemea michuano hiyo kuanza "mapema kadri itakavyokuwa inawezekana".
Klabu nyingine tatu zaidi zilizo katika kundi la waasisi, zitangazwa baadaye, ilisema ESL katika taarifa yake, huku nafasi nyingine tano zikipatikana katika michuano ya kufuzu kila mwaka.
Klabu 15 zilizoasisi zitahakikishiwa nafasi ya kushiriki Super League kila mwaka.
Klabu zitagawanywa katika makundi mawili ya timu 10 ambazo zitacheza nyumbani na ugenini. Timu zitakazoshika nafasi tatu za juu katika kila kundi, zitafuzu kucheza robo pamoja na timu zitakazoshika nafasi ya nne na ya tano ambazo zitapambana katika mechi za mtoano kuamua nafasi mbili zilizosalia katika robo fainali.
Baada ya hapo, ligi hiyo itaendelea na mfumo wa mtoano kwa mechi za nyumbani na ugenini kabla ya kupata timu mbili zitakazocheza fainali ambayo itakuwa ya mechi moja tu.
Kwa upande wa mapato ya klabu, waandaaji wanasema zitapata "malipo ya mgawo" ambayo yatakuwa makubwa kuliko yanayopatikana hivi sasa katika michuano ya Ulaya.
Kwa kusaini kushiriki ligi mpya, "klabu zinazoasisi zitapata Euro 3.5 bilioni (sawa na Sh9.79 trilioni za Kitanzania) kwa ajili ya kusaidia mipango ya uwekezaji katika miundombinu na kutatua matatizo yaliyotokana na athari za janga la Covid-19," inasema taarifa hiyo.

'Mradi wa ubinafsi'
Klabu za ESL zimetuhumiwa kuwa na ubinafsi, zikipondwa na viongozi wa Uingereza na Ufaransa na kutishiwa kutengwa kimataifa.
Licha ya ahadi yao ya kuendelea kushiriki ligi za nchi zao, Chama cha Soka Ulaya (UEFA) na mamlaka za soka za nchi tatu, zimeonya kuwa klabu zitakazohusika zitafungiwa kushiriki michuano ya ndani na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
"Tutaendelea kuwa pamoja katika kuzuia mradi huu wa ubinafsi, mradi ambao umeasisiwa kwa maslahi binafsi ya klabu chache katika wakati ambao jamii inahitaji mshikamano zaidi kuliko wakati mwingine wowote," taarifa ya pamoja ilisema.
UEFA pia imetishia kuwa wachezaji wa klabu zitakazoshiriki, "watanyimwa fursa ya kuchezea timu zao za taifa".
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson alisema klabu hizo hazina budi "kujibu swali kwa mashabiki wao na jumuiya kubwa zaidi ya soka kabla ya kuchukua hatua nyingine yoyote".
Kukiwa hakuna klabu kutoka Ufaransa kati ya hizo za mwanzo za ESL, Rais Emmanuel Macron alisema mpango huo una hatari ya "kutishia kuua kanuni za mshikamano na faida za kimichezo".
Tangazo la ESL lililenga kuiwahi UEFA ambayo pia imepanga kutangaza kubadilisha muundo wake leo, ikiongeza idadi ya timu kutoka 32 hadi 36, na nafasi mbili kwa klabu nyingine zitakazoingia kwa mpango maalum. Kutakuwa na mechi zisizopungua kumi kwa kila timu.
Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) lilieleza kutouidhinisha mpango huo na kutaka pande zote kuhusishwa kwa mazungumzo ya utulivu, ya kujenga na yenye uwiano kwa ajili ya nia njema kwa mchezo wa mpira wa miguu."
Ligi Kuu ya England, ambayo ni tajiri kuliko zote barani Ulaya, ilitoa taarifa kali.
"Mashabiki wa klabu yoyote nchini England na bara lote la Ulaya wanaweza kuota kwa sasa kuwa klabu zao zinaweza kupanda hadi kileleni na kucheza dhidi ya timu bora," ilisema taarifa yake.
"Tunaamini kwamba wazo la Super League ya Ulaya litaua ndoto hii."
Arsenal, ambayo kwa sasa inashika nafasi ya tisa katika Ligi Kuu-- ikiwa mbali na nafasi za kufuzu kucheza mashindano ya Ulaya-- ilidokeza uwezekano wa kuwepo vikwazo ikisema "kuna mengi ya kufanya ili kuwezesha mashindano kuwa na uhai".
Chama cha Klabu za Ulaya (ECA) kilisema kinapinga vikali mpango wa kuanzisha Super League ya Ulaya.
Juventus, ambayo rais wake Andrea Agnelli pia ni kiongozi wa ECA, imesema kiongozi wake na klabu walijiondoa.
Klabu hiyo ilionya kuwa "haiwezi kutoa uhakikisho kuwa hatimaye mradi huo utazinduliwa kwa mafanikio".
Juventus inapambana kuhakikisha inamaliza msimu ikiwa katika nafasi nne za juu nchini Italia na AC Milan, ambayo imeshatwaa ubingwa mara saba, haijashiriki Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2014.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, ambaye alitangazwa kuwa rais wa kwanza wa ESL, alisema ligi hiyo mpya inaonyesha utashi wa klabu.
"Soka ni mchezo pekee duniani wenye zaidi ya mashabiki bilioni nne na wajibu wetu kama klabu kubwa ni kufanyia kazi utashi wao," alisema.

New Content Item (1)
New Content Item (1)


Mwenyekiti mwenza wa Manchester United, Joel Glazer, ambaye atakuwa makamu mwenyekiti wa Super League, alisema michuano hiyo "itafungua ukurasa mpya wa soka barani Ulaya".
Klabu hizo pia zilisema ligi ya wanawake pia itaanzishwa.

Klabu za Ujerumani, Ufaransa nje
Klabu za Ufaransa na Ujerumani, wakiwemo mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich na PSG iliyofika fainali msimu uliopita, hazimo katika klabu asisi za ESL.
"Tunazishukuru klabu hizo, hasa za Ufaransa na Ujerumani, ambazo zimekataa kutia saini (makubaliano haya)," ilisema UEFA.
Rais wa La Liga, Javier Tebas alizilinganisha klabu zilizosaini ESL na mlevi anayeondoka baa saa 11:00 jioni akiwa "amelewa ubinafsi na kukosa mshikamano".
Kiongozi wa Ligi ya Ujerumani, Christian Seifert alisema ligi hiyo mpya "itafanya uharibifu usiorekebishika kwa ligi za taifa za nchi".


Vidokezo Super League

Idadi ya timu ni 20
Klabu zilizothibitisha hadi sasa ni 12: Manchester United, Liverpool, Arsenal, Chelsea, Manchester City, Tottenham (England), Barcelona, Real Madrid, Atletico Madrid (Hispania), Juventus, AC Milan, Inter Milan (Italia)
Muundo: Makundi mawili yenye timu 10; timu zitakazoshika nafasi tatu za juu zitafuzu kucheza robo fainali, kutakuw ana mechi za mtoano baina ya timu zitakazoshika nafasi za nne na tano kupata timu mbili zitakazokamilisha robo fainali.
Tarehe ya kuanza: "Mapema kadri mradi utakavyokuwa unawezekana"; kwa mwaka ni Agosti
Idadi ya makombe yaliyotwaliwa na timu 12 zilizotia saini kushiriki ni 40
Rais wa Ligi: Florentino Perez (Real Madrid)
Makamu wa Rais: Andrea Agnelli (Juventus) na Joel Glazer (Manchester United).