Kisa Madrid, PSG yampa mkataba mpya Mbappe

WAKATI tetesi za kuondoka kwake zikiwa zinazidi kupamba moto, Mabosi wa Paris St-Germain wanadaiwa kumpa mkataba mpya wa miaka miwili mshambuliaji wao Kylian Mbappe ikiwa ni sehemu ya kumzuia asiondoke dirisha lijalo na anahusishwa kujiunga Real Madrid.

Mkataba huo mpya unadaiwa kuwa na thamani ya Pauni 136 milioni ambazo ni mjumuisho wa pesa atakazopata Mbappe kutokana na mshahara na bonasi ya usajili.

Kupitia tovuti ya AS, inaelezwa Mbappe (25), ameshafanya uamuzi wa kuondoka PSG mwisho wa msimu na kutua Madrid, lakini mabosi wa PSG hawataki kukubaliana na hilo.

Mkataba wa sasa wa Mbappe unamalizika mwisho wa msimu huu na alihusishwa kuondoka tangu mwanzo wa msimu lakini ilishindikana.

Staa huyu mara kadhaa katika kipindi cha hivi karibuni amekuwa akihusishwa na Liverpool ingawa inaonekana kuwa ngumu kutua huko kwa sababu ya ndoto yake ya kuichezea Madrid.