Kipigo cha Man City chamwamsha ten Hag

Kipigo cha Man City chamwamsha ten Hag

MANCHESTER ENGLAND.  ERIK ten Hag amechukia, amewambwatukia mastaa wake wa Manchester United akiwaambia ‘haikubaliki’baada ya kukubali kichapo cha kudhalilisha kutoka kwa mahasimu wao, Manchester City kwenye mchezo wa Ligi Kuu England juzi Jumapili huko Etihad.

Mdachi huyo aliyechukizwa na kikosi chake alisema wachezaji wake walikuwa hovyo kwelikweli na hivyo kuamua kumweka benchi Cristiano Ronaldo kwa heshima ili asidhalilike.

Ten Hag aliishiwa maneno kuelezea kiwango cha timu yake kwenye kipindi cha kwanza ambapo Man City ilikuwa mbele kwa mabao 4-0 na alichosema ni hiki hapa: “Ni rahisi tu, kutojiamini. Hatukuonyesha nguvu yetu, tulifanya makosa ya kiufundi tukaadhibiwa. Unapokosa kujiamini uwanjani, huwezi kushinda mechi, hali hii haikubaliki.”

Ten Hag alimtoa Marcus Rashford na kumwingiza Anthony Martial kwenye dakika ya 59, ambapo Mfaransa huyo alifunga mara mbili kwenye kipigo hicho cha mabao 6-3.

Bosi huyo wa Old Trafford alisema si kwamba alimchunia Ronaldo kwa kutomchezesha kwenye mechi hiyo, bali alilinda hadhi yake kwenye mechi hiyo ambapo mashabiki wa Man United walikuwa wamechukia na kuondoka kabla hata ya filimbi ya mapumziko.

Ten Hag alisema: “Nisingeweza kumwingiza kwa heshima ya Cristiano, kwa heshima ya maisha yake ya soka. Kitu kingine ni faida ambayo tumeipata kwa kumwingiza Martial, alihitaji dakika kadhaa za kuwamo uwanjani. Lakini, sitaki kuzungumzia hilo.”

Ten Hag hasira zake ni kwa wachezaji wake kucheza kizembe na kumruhusu Erling Haaland afunge hat-trick yake ya tatu kwenye ligi uwanjani Etihad, huku Phil Foden naye akipiga hat-trick katika mchezo huo.

Kocha huyo Mdachi alisema: “Niliwaambia wachezaji wangu walikosa kujiamini. Tuliwaacha wacheze. Lazima tukosoane na kuelewa kabisa walichofanya wachezaji wangu, kujiamini uwanjani, kucheza staili yetu. Imenihuzunisha sana.”

Man United ilishinda mechi nne mfululizo tangu ilipochapwa 4-0 na Brentford, lakini Ten Hag alikiri yale mambo ya zamani, tabia za hovyo za mastaa wake vilijirudia kwa Man City.

Aliongeza: “Katika mechi nne zilizopita tulikuwa na ari mno uwanjani, tulikuwa tunajiamini. Hapa, mambo yamekuwa kinyume chake. Sawa ni kawaida kwenye mpango wowote kukumbana na vikwazo. Lazima tumejifunza, lakini ukweli ni heri ufahamike. Hatuwezi kulinyamazia hili, kama tutafanya hivyo, basi hatuwezi kupata suluhisho, lazima tuzungumze.”

Kocha Ten Hag alimtetea kiungo wake Christian Eriksen akisema: “Kila mtu anadhani ni siku mbaya ofisini. Tulikosa hali ya kujiamini na kucheza mpira kuanzia nyuma, tukawafanya wao kuwa imara. Kuna mambo kibao tunapaswa kubadilika, mengi mengi yanahitaji kufanya vizuri uwanjani. Ile kitu haikubaliki kabisa.”