KIJIWE CHA SALIM: Lacina The Big Tree aliyeacha darasa la uungwana Viwanja vya soka

Muktasari:

  • Kikosi hicho kililinganishwa kwa mbali na cha Brazil  miaka ya 1970 kinachozungumzwa hadi leo kuwa timu nzuri ya soka kuwahi kuchomoza duniani. Miongoni mwa wachezaji wa Brazil ni Edson Arantes do Nascimento (Pele), Eduardo Tostao, Felix Alberto, Jair Jiarzinho, Colodoaldo Santana, Roberto Rivelino, Carlos Alberto, Roberto Miranda na Jose Fontana.

KIPINDI cha kuingia kwa karne ya 21 wakati ilipoanza Ivory Coast, ilisifika Bara la Afrika na nje kwa kuwa na kikosi wa soka kilichoitwa kizazi cha dhahabu.

Kikosi hicho kililinganishwa kwa mbali na cha Brazil  miaka ya 1970 kinachozungumzwa hadi leo kuwa timu nzuri ya soka kuwahi kuchomoza duniani. Miongoni mwa wachezaji wa Brazil ni Edson Arantes do Nascimento (Pele), Eduardo Tostao, Felix Alberto, Jair Jiarzinho, Colodoaldo Santana, Roberto Rivelino, Carlos Alberto, Roberto Miranda na Jose Fontana.

Katika kikosi cha dhahabu cha Ivory Coast kilichoongozwa na Didier Drogba walikuwemo wachezaji wa klabu za nchi za Ulaya, Asia na Qatar. Kati ya waliosifika ni Didier Drogba, ndugu wawili Yaya na Kolo Toure Didier Zokora, Emmanuel Ebou, Salomon Kalou, Gervais Yao, Kouassi Keita, Abdul Kader na Wilfred Bony.

Lakini alikuwepo mchezaji mmoja aliyetoa mchango mkubwa katika kikosi hicho, ila hakupata bahati ya kutajwa sana labda kwa vile ni mpole, hapendi kujitutumua na mara chache huzungumza na vyombo vya habari.

Huyo alikuwa ni mshambuliaji Lacina Emeghara Traore ambaye maarufu kwa jina la The Big Tree (mti mkubwa) kutokana na umbile la urefu wa futi 6 na inchi 5 na uzito wa kilo 93.

Miongoni mwa sifa zake zilikuwa ni kupasua ngome ya wapinzani kwa kishindo na alipopata nafasi ya kutingisha nyavu alimpasia mwenzake kufanya hivyo.

Kila alipoulizwa kwa nini hakufunga bao wakati angeweza kufanya hivyo, jawabu la Traore lilikuwa kwamba dini ya Kiislamu imemfundisha kila akiwa na kitu kizuri anatakiwa ampe mwenzake kama zawadi ili kuimarisha udugu.

Alisema ni muhimu kwa ndugu kushikamana na alipata mafunzo hayo kwa vile alikuwa na ndugu wa kiume 16 na wa kike 14.

Traore ambaye alichezea klabu zaidi ya 10 nyumbani na nje na 2022 alikuwa Varzim S.C ya Ureno alizaliwa Abidjan, Mei 20, 1990.

Baada ya kusakata chandimu mitaani alijiunga na Chuo cha Soka cha Klabu ya Asec Mimosas jijini Abdijan na kuwa nayo kwa miaka minne hadi Januari 2008 alipojiunga na CFR Cluj ya Romania. Hii ilikuwa baada ya kuichezea Stade d’Abidjan michezo 47 na kuifungia mabao 18 msimu wa 2007–2008.

Mnamo Februari 2011, Traoré alikwenda Klabu ya Kuban Krasnodar iliyopo pembezoni mwa mto Kuban, Kusini mwa Russia na huko alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi wa mwezi wa Mei.

Ilipofika Juni 2012 alihamia Anzhi Makhachkala ya Russia na kuwa mmoja wa wafungaji wake bora katika Ligi Kuu Russia na Ulaya.

Baada ya hapo aliichezea Monaco 2014 na hakuchukua muda mrefu akarudi Anzhi Makhachkala na baadaye kuichezea Everton baada ya kukataa ombi la kutakiwa na West Ham United. Wakati huo alikuja kusumbuliwa na maumivu ya misuli na kukaa nje kwa muda na alipopona akajiunga mara nyingine na Monaco.

Alirudi Russia 2016 kujiunga na CSKA Moscow kwa mkopo, lakini alikaa nayo kwa muda mfupi na kwenda pia kwa mkopo Sporting Gijon ya Hispania na kuwika katika Ligi Kuu ya nchi hiyo, La Liga.

Mwezi Agosti mwaka huo Traore alijiunga na Amiens SC ya Ufaransa kwa mkopo na miaka miwili baadaye alikwenda Hungary kuichezea Újpest FC. Baada ya kuwa na klabu hiyo kwa miaka miwili huku akisumbuliwa na maumivu alirudi Romania kuichezea CFR Cluj.

Wakati wote akiwa na klabu hizo Traore alikuwa akiitwa kujiunga na timu ya taifa ya Ivory Coast ya vijana na baadaye ya taifa katika mashindano ya Afrika, Olimpiki na Kombe la Dunia.

Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger aliwahi kutaka kumsajili kwa kitita cha Pauni 3.6 milioni, lakini alikataa. Traore aliichezea Ivory Coast michezo 13 na akasema hawezi kusahau mchezo ulioipatia nchi yake Kombe la Mataifa ya Afrika 2015 baada ya kuishinda Ghana kwa penalti 9-8.

Katika mchezo huo timu hizo zilimaliza muda wa nyongeza bila ya kufungana. Traore alisifika kwa kufanya juhudi kubwa kutingisha wavu wa Ghana, lakini haikuwa bahati yake na alimlaumu kipa wa Ghana, Brimah Razak kwa kumnyima raha kutokana na kupangua mikwaju yake mitatu aliyotumaini ingetikisha nyavu.

Siku hizi huonekana mara nyingi huonekana katika mihadhara ya dini na mara chache hufika katika viwanja vya mpira na hasa pale Ivory Coast inapokuwa na mchezo wa kimataifa katika uwanja wa nyumbani.