Kadi ya bluu yasitishwa

Mchezaji akionyeshwa kadi hiyo atatoka nje ya uwanja kwa dakika 10 na kisha kurejea mchezoni. Kadi hiyo itatolewa kwa makosa mawili tu, kufanya faulo (ambayo haikidhi vigezo vya kuonyeshwa kadi nyekundu) katika kuzuia mipango ya kuanzishwa kwa shambulizi na kupinga uamuzi wa waamuzi.  

ZURICH, USWISS. MCHAKATO wa uanzishaji wa sheria ya matumizi ya kadi ya bluu, yamesitishwa baada ya kukosolewa na wadau wengi ikiwamo Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Awali, shirikisho linalotunga sheria za soka duniani (IFAB), lilipanga kutangaza ujio wa kadi hiyo ijumaa ya wiki iliyopita, kabla ya kusitisha  na sasa inasubiri kufanyika kwa kikao cha mwaka  na mapendekezo ya sheria mbalimbali yatawasilishwa na kujadiliwa, kwa mujibu wa ESPN.

Mpango wa kuanzisha kadi ya bluu ilikuwa ni kuweka usawa kwenye makosa mbalimbali na mchezaji ataonyeshwa kadi hiyo na kutakiwa kukaa nje ya uwanja kwa dakika 10, ikiwa kosa hilo ni zaidi ya lile la kuonyeshwa kadi ya njano na dogo la kuonyeshwa  kadi nyekundu.

Wakati IFAB ikipanga kuanzisha majaribio ya kadi katika baadhi ya maeneo, FIFA imetoa taarifa inayoeleza hawajaafiki juu ya suala hilo.

Licha ya kwamba wachezaji walikuwa wakitolewa nje kutokana na makosa yao, lakini hapo awali waamuzi hawakuwa na kadi yoyote kati ya njano au nyekundu hadi ilipofikia kwenye Kombe la Dunia mwaka 1970 na kadi ziliingizwa rasmi.