Joshua, Fury ngoma ngumu

HADI juzi Jumatatu hakukuwa na uhakika wa kusainiwa kwa mkataba wa pambano la mabondia Waingereza Tyson Fury na Anthony Joshua waliopo kwenye uzito wa juu duniani (heavyweight).

Sababu kubwa iliyochelewesha mkataba huo kusainiwa ni ishu za muingiliano uliopo wa mabondia hao ambao kila mmoja kwa ukubwa wa chapa yake ana makubaliano binafsi ya kimkataba na taasisi za kuonyesha mapambano yanayomhusu.

Hiyo ni mbali na kila mmoja kuwa na usimamizi wa mapromota na taasisi, kiasi cha bondia mwenye nguvu kwenye pambano baina yao kwa sasa Fury kutishia kuachana na mpango wa kupigana na Joshua akihisi upande wake kuwa sababu.

Kuonyesha kwamba hataki masihara na anataka zipigwe, Fury alimpatia nafasi ya mwisho hadi jana Jumanne awe amekamilisha vitu vyake, huku Joshua akisisitiza kusaini kwake ni suala dogo, ila kilichokwamisha ni ishu za kisheria na maslahi ya pande mbili hususan kampuni zenye haki ya kuonyesha mapambano. Taarifa rasmi ya pambano hilo ilitarajiwa kutolewa kati ya jana au leo.