Huku Porto na Arsenal, kule Napoli na Barcelona

PORTO, URENO. MAMBO ni moto. Arsenal itarusha kete yake ya kwanza kwenye mtoano wa hatua ya 16 bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati itakapoifuata FC Porto huko kwenye Uwanja wa Estio do Dragao usiku wa leo Jumatano.

Kwenye hatua ya makundi, Arsenal ya Mikel Arteta ilizoa pointi 13 kati ya 18, tena ilipangwa na timu ngumu za PSV, Sevilla na Lens, hivyo wataifuata Porto ikiwa na imani kubwa ya kutoboa kwenye hatua inayofuata. Lakini, Porto yenyewe ilimaliza na pointi 12 kwenye hatua ya makundi, huku ikiwa ilipangwa pamoja na miamba ya Ulaya, Barcelona.

Jambo hilo linafanya mchezo huo wa usiku wa leo kuwa na ushindani zaidi kutokana na kila tumu kujaribu kusonga mbele. Arsenal imefeli mara kadhaa kuvuka kwenye hatua ya 16 bora, hivyo itahitaji kufanya kweli safari hii.

Rekodi zinaonyesha Porto na Arsenal zimekutana mara sita kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na wababe hao wa Ureno wameshinda mara mbili, huku The Gunners ikishinda tatu na mechi moja ilimalizika kwa sare.

Kipute kingine cha mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kitakachopigwa usiku wa leo, Barcelona itakuwa ugenini kukipiga na Napoli kwenye Uwanja wa Diego Armando Maradona huko Naples, Italia.

Kwenye raundi hiyo ya mtoano kwenye michuano ya Ulaya, Barcelona na Napoli zimekutana mara kadhaa na katika msimu wa 2021/22, Barca ilishinda vita kwa jumla ya mabao 5-3, huku zilikutana pia kwenye hatua ya 16 bora katika msimu wa 2019/20 na miamba hiyo ya Nou Camp, ilitamba ikivuka kwa jumla ya mabao 4-2. Safari hii itakuwaje? Ngoja tuone.