Haller kutoka kuugua saratani hadi kuipa Ivory Coast taji la Afcon

Muktasari:

  • Sebastien Haller alizaliwa Ufaransa mwaka 1994, mama yake akiwa ni raia wa Ivory Coast huku baba yake akiwa ni raia wa Ufaransa.

Jina la Sebastien Haller limekuwa gumzo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) uliochezwa jana huko Ivory Coast na timu ya taifa ya nchi hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nigeria.

Kutajwa kwa jina la Haller kumetokana na nyota huyo anayeichezea Borussia Dortmund ya Ujerumani kufunga bao lililoihakikishia ushindi timu yake ya taifa na kuiwezesha kushinda taji la Afcon kwa mara ya tatu.

Kabla ya hapo, William Trost Ekong aliifungia Nigeria bao la kuongoza, lakini baadaye, Franck Kessie akaisawazishia Ivory Coast, na alikuwa ni Haller ambaye alileta heshima nyumbani kwa kufunga bao la pili na la ushindi.

Kwa Haller, bao hilo linaweza kubeba kumbukumbu kubwa ya nyakati ngumu alizopitia katika maisha yake hadi kuwa shujaa wa taifa, ambazo zinaonyesha roho ya ujasiri na uvumilivu ambayo nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 amepitia.

Kama sio uimara wa kuhimili magumu aliyopitia, pengine leo hii nyota huyo asingekuwa sehemu ya mafanikio ya Ivory Coast ama kwa kutokuwa sehemu ya kikosi au kuwepo kaburini.

Julai 2022, nyota huyo mzaliwa wa Ufaransa alibainika kuwa na tatizo la saratani ya tezi dume na kuanza kupatiwa matibabu ambayo yalimlazimisha kuwa nje ya uwanja kwa muda.

Matibabu hayo  yalimuendea vizuri na hatimaye Januari 2023 alirejea uwanjani kuitumikia Borussia Dortmund na timu yake ya taifa ya Ivory Coast.

Mwaka mmoja baadaye, nyota huyo amekuwa lulu kwa taifa lake baada ya kuifungia bao la ushindi timu yake ya taifa katika mchezo wa fainali ya Afcon dhidi ya Nigeria ambao Ivory Coast iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutwaa taji.

Ikumbukwe ni huyohuyo Sebastien Haller aliyeivusha Ivory Coast kuingia hatua ya fainali baada ya kufunga bao pekee la ushindi katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya DR Congo.


Shukrani kwa baba Mzungu

Katika hali ya kushangaza, mama wa Sebastien Haller ambaye ndiye Muivory Coast hakupendezwa na mwanawe kujihusisha na soka na badala yake alimtaka ajikite zaidi na masomo.

Lakini baba wa mshambuliaji huyo ambaye ni raia wa Ufaransa, alionekana kumuunga mkono kijana wake kwa kumpatia vifaa na kumsapoti hadi alipofikia ngazi ya kuwa mchezaji mwenye jina kubwa.

Leo hii nyota huyo ameandika historia katika taifa la mama yake ambaye awali hakumtaka acheze soka pasipo kulinufaisha taifa la baba yake aliyempa sapoti kubwa hadi anafika hapo alipo.


Klabu alizopitia,

Auxerre- 2007-2015

Utrecht- 2015-2017

Eintracht Frankfurt- 2017-2019

West Ham United- 2019-2021

Ajax- 2021-2022

Dortmund- 2022 hadi sasa.