Guardiola kunasa majembe Januari
Muktasari:
- Kocha huyo Mhispaniola atakabidhiwa fungu la kutosha kwa ajili ya usajili baada ya kutumia zaidi ya Pauni 250 milioni kwenye kuwanasa wachezaji wapya katika kipindi cha miaka miwili.
MANCHESTER, ENGLAND: PEP Guardiola anajiandaa kupiga bei mastaa kadhaa kwenye dirisha la Januari ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka saba aliyokuwa kwenye kikosi cha Manchester City.
Kocha huyo Mhispaniola atakabidhiwa fungu la kutosha kwa ajili ya usajili baada ya kutumia zaidi ya Pauni 250 milioni kwenye kuwanasa wachezaji wapya katika kipindi cha miaka miwili.
Kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes na mwingine Martin Zubimendi wa Real Sociedad wapo kwenye rada ya Man City wakihitaji huduma zao baada ya kumpoteza mshindi wa Ballon d’Or, Rodri kwa msimu mzima baada ya kuumia gotu.
Man City imepoteza mechi saba kati ya 10 za mwisho na kikosi hicho kimekuwa kikiandamwa sana na majeruhi na kuwa kwenye hali mbaya. Hivyo, mpango uliopo ni kuingia sokoni wakati dirisha litakapofunguliwa ili kunasa wachezaji watakaokuja kunusuru hali ya mambo yanavyokwenda kwenye msimu wao.
Man City inafahamu wazi ugumu wa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu kwenye dirisha la Januari na wamekuwa hawafanyi usajili kwenye dirisha hilo la majira ya baridi tangu walipofanya hivyo kwa beki wa kati Aymeric Laporte mwaka 2018.
Na sasa bodi ya Man City itamsapoti Guardiola kama kutakuwa mchezaji mzuri anapatikana kwenye dirisha hilo la Januari bila ya kujali bei anayouzwa.
Kiungo Bruno inaaminika kwamba atavutiwa na uhamisho wa kwenda Man City, lakini kuwakabili Newcastle United wamwaachie staa wao huyo katikati ya msimu ni jambo gumu.