Chelsea yaweka rekodi Ulaya

LONDON, ENGLAND. MABAO ya Timo Werner  na Mason Mount, yalitosha kwa Chelsea  kuitupa nje Real Madrid na kutinga fainali ya  Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikiandikwa  rekodi ya  kuwa klabu ya kwanza timu zake mbili, Wanaume na Wanawake  kufika hatua hiyo.

Vijana wa Thomas Tuchel wametinga fainali ambayo watacheza dhidi ya Manchester City mwishoni mwa mwezi huu huko Uturuki baada ya kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 3-1, wakiwa nyumbani, jana waliitandika Real Madrid kwa mabao 2-0.

Ushindi huo uliwafanya vijana hao wa Tuchel kuungana na timu yao ya Wanawake inayonolewa na Emma Hayes zote kwa pamoja kutinga fainali ya mashindano hayo makubwa, Chelsea ya Emma ilitinga hatua hiyo baada ya kuitandika timu ya Wanawake ya  Bayern Munchen kwa jumla ya mabao 5-3.

Akiongelea mafanikio ambayo wameyafikia ya kutinga fainali mbili, ikiwemo ya Kombe la FA,  Tuchel amesema  
kazi bado haijamalizika.
,"Tunatakiwa kwenda fainali tukiwa kwenye ari nzuri, bado kazi hatujamaliza, tunatakiwa kwenda kutwaa ubingwa,"

"Najivunia, walistahili kushinda usiku wa leo (jana). Walitufanya kuhangaika lakini tulikuwa hatari na hatukupoteza njaa na umakini kwenye kujilinda,"

"Kilikuwa kiwango bora na kama tungekuwa makini tungefunga mabao mengi zaidi lakini huu sio wakati wa kuanza kukosoa, haya ni mafanikio makubwa," amesema.

Kitendo cha Tuchel kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya  na Chelsea ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kufika hatua hiyo misimu miwili mfululizo akiwa na timu mbili tofauti. Haijawahi kotokea tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.

"Nina furaha kubwa sana kuyafikia mafanikio haya kwenye maisha yangu ya soka," amesema kocha huyo ambaye msimu uliopita alitinga hatua hiyo akiwa na PSG.