Chelsea yashindwa kuvunja mwiko

LONDON, ENGLAND
HAKUNA mbabe. Ndio unaweza kusema hivyo wakati kipyenga cha mwisho kinapulizwa pale kwenye dimba la Stamford Bridge, London na mchezo kati ya Manchester United dhidi ya Chelsea kumalizika kwa suluhu ya 0-0.


Chelsea ndio imeendelea kuwa na matokeo mabaya mbele ya Man United kwani tangu mwaka 2017 haijawahi kupata ushindi dhidi ya wababe hao zaidi katika mechi tano za mwisho imetoa sare mbili na ikafungwa tatu.


Mchezo huo ulioanza saa 1:30 usiku ulikuwa wa aina yake kwani timu zote zilijaribu kufanya mashambulizi kwa kupokezana, lakini tatizo lilikua ni kwenye kukwamisha mpira wavuni.


Chelsea ndio ilionekana zaidi kumiliki mpira lakini hakukuwa na mashambulizi ya hatari zaidi iliyoelekeza kwenye lango la Man United ambayo ilijihami muda mwingi na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.


Kwa matokeo hayo Chelsea imeendelea kusalia kwenye nafasi ya tano ikiwa na alama 44 baada ya kucheza mechi 26, vile vile Man United imeendelea kusalia kwenye nafasi ya pili kwa alama zake 50 ilizokusanya kwenye mechi 26.