Chelsea, Man City zisahau kwa Lukaku

Wednesday July 28 2021
lukaku pc

MABOSI wa Inter Milan wamesisitiza kwamba staa wao kutoka Ubelgiji, Romelu Lukaku  hauzwi katika dirisha hili licha ya timu kibao kuonyesha nia ya kuhitaji kumsainisha.
Lukaku, 28, alionyesha kiwango bora kwa msimu uliopita ambapo  alifunga mabao 24  kwenye 36 za Ligi Kuu Italia.
Kiwango chake kiliisaidia Inter kwenye harakati za kuuchukua ubingwa wa kwanza wa Seria A tangu mwaka 2010.
Fundi huyu kutoka Ubelgiji amekuwa kwenye rada za timu nyingi kubwa barani Ulaya ikiwa pamoja na  Chelsea na Manchester City ambazo zinapigana vikumbo ili kuhakikisha zinaipata saini yake katika dirisha hili.
Katika mazoezi ya maandalizi ya msimu ujao mtendaji mkuu wa Inter Beppe  Marotta alisisitiza kwamba mchezaji huyo ni muhimu kwenye timu, hivyo licha ya hali mbaya ya kiuchumi wanayopitia kwa sasa hawapo tayari kumuuza.
"Kwa upande wetu, tunaweza kusema ndio hatumuuzi. Huyu ni mchezaji muhimu sana kwa kocha wetu  Simone Inzaghi."
Lukaku amegeuka lulu tangu atue kwenye viunga vya Italia katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2019 akitokea Man United ambapo hadi sasa amefunga mabao 64 akiwa na wababe hao.
Kiwango alichoonyesha kwenye michuano ya Euro akiwa na Ubelgiji pia kimeonekana kuzidi kuzivutia timu zinazomuhitaji.
Chelsea imekuwa ikihitaji kumsainisha Lukaku kama mbadala wa straika kutoka Borussia Dortmund Erling Haaland ambaye dili lake lina asilimia chache za kukamilika.
Sababu moja wapo ya dili la  Haaland  kusua sua ni kutokana na kiwango kikubwa cha pesa kinachohitajika na mabosi wa Dortmund.
Hata hivyo mapema mwaka huu Inter iliweka wazi kwamba inahitaji kuuza baadhi ya wachezaji wake katika kikosi cha kwanza ili kukabiliana na ukata lakini imepigia mstari jina la Lukaku kwamba haimuuzi.
Aidha tayari imeshapokea Pauni 51.3 milini kutoka kwa Paris Saint-Germain baada ya kumuuza Achraf Hakimi, kiasi ambacho kimeripotiwa kushibisha mifuko yao kwa kiasi fulani kutokana na hali yao ya kiuchumi.
Kwa upande wa Manchester City yenyewe imekuwa ikihitaji kumsajili ili akawe mbadala wa  Sergio Aguero aliyejiunga na Barcelona akiwa mchezaji huru katika dirisha hili.
Man City ilijaribu kutaka kumsainisha Haaland lakini ilishindwa kutokana na pesa ndefu inayohitajika na badala yake imeamua kuhamia kwa staa huyo inayeamini hatauzwa kwa pesa ndefu.
Licha ya kauli hiyo Chelsea bado inaonekana kuendelea na harakati kwani kulikuwa na mapungufu makubwa kwenye eneo lao la ushambuliaji kwa msimu uliopita hivyo inahitaji kuliboresha ili kuhakikisha inafanya vizuri msimu ujao.
Chelsea ilimsajili Timo Werner ambaye alikuwa akitegemewa kuonyesha kiwango bora, hatma yake mambo yakawa mabaya tofauti na ilivyotegemea.
Vilevile inataka kumuuza Tammy Abraham anayehitajika na Arsenal, hivyo pesa itakayomuuzia inatarajia kuongeza na kufanya usajili wa aidha Haaland ama Lukaku.


Advertisement