Bruno asubiri namba mpya

MANCHESTER, ENGLAND. FUNDI wa mpira, Bruno Fernandes anajiandaa kukabidhiwa namba mpya ya jezi kwenye kikosi cha Manchester United kwa msimu ujao, baada ya anayeimiliki namba hiyo kwa sasa kumaliza mkataba wake baadaye mwezi huu.

Kiungo huyo Mreno, Fernandes tangu alipotua Man United kutoka Sporting Lisbon amekuwa akivaa jezi Namba 18. Fernandes alichukua namba hiyo iliyowahi kuvaliwa na Paul Scholes pia na hajabadili tangu alipojiunga kwa ada ya Pauni 46.6 milioni, Januari 2020.

Lakini, kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, jezi Namba 8 itakuwa wazi kutokana na kiungo Mhispaniola, Juan Mata kuwa kwenye siku za mwisho kabisa za kuachana na maisha ya Old Trafford.

Mata, amekuwa hachezeshwi sana kwa siku za karibuni na kinachoelezwa ni kuna timu za nje ya England zinahitaji saini yake. Kilichopo ni anaweza kurudi kwao Hispania au akatimkia Marekani.

Man United ina nafasi ya kumwongeza mkataba wake kwa mwaka mmoja zaidi, lakini kinachoelezwa watamuuliza mwenyewe kama anataka kubaki au kuondoka. Kama ataondoka, basi Namba 8 itakuwa wazi kwa ajili ya Fernandes kuichukua. Bila ya shaka kiungo Fernandes atakubali kuichukua namba hiyo akitakiwa kufanya hivyo.

Namba 8 ni jezi aliyovaa kote, alipokuwa Udinese na Sporting Lisbon, lakini ilishindikana wakati anatua Old Trafford kwa sababu ilikuwa na mtu na hivyo aliamua kuchukua Namba 18 na kutoa sababu zake.

Fernandes alisema: “Kuna sababu nyingi za kuchukua Namba 18. Ni namba ninayoipenda. Miaka mitatu iliyopita nilikuwa navaa jezi Namba 8 kwa sababu ni namba ya baba yangu alipokuwa mchezaji na pia ni ya siku yangu ya kuzaliwa, hivyo ni namba niliyoipenda.

“Namba 18 pia ni siku ya kuzaliwa ya mke wangu na sababu nyingine wakati nakua nilikuwa namshangilia Paul Scholes na alivaa namba hii.”