BATTLE OF THE TITANS

MAISHA yanakwenda kwa kasi sana. Leo kutakuwa na mechi kati ya Manchester United na Liverpool halafu hakuna shabiki atakayeruhusiwa kuingia uwanjani.

Hii ina maana kile kikundi cha mashabiki wachache kutoka Goodson Park chenye wanadamu wenye damu za Everton hakitapata fursa ya kuzomea wale wanaume 11 wa Liverpool kama ilivyokuwa utaratibu wao kwa kuwa ni mahasimu wao.

Lakini hiyo haiondoi uhondo wa mchezo huu ambao kwa zaidi ya miaka 30 sasa haujawahi kupoteza mvuto.

Kwa muda kirefu chama cha soka nchini England kiliamuru mechi hii ichezwa mchana ili kuepuka maafa ya watu kupoteza maisha kwa sababu ya vurugu zilizotokea hapo awali wakati mechi hii inapingwa.

Inawezekana vurugu zilichagizwa zaidi na aina ya wachezaji waliokuwa wanazichezea timu hii hapo awali, upande wa Man United kulikuwa na mtukutu, Eric Cantona bila kumsahau kipa mwenye vituko Peter Schmeichel na Liverpool kulikuwa na mbabe Emile Heskey.

Muda huu inawezekana isiwe mechi ya vurugu kutokana na aina ya wachezaji waliopo kwa timu zote mbili lakini bado ni mechi inayovuta hisia za mashabiki wengi kwa kuwa inazikutanisha timu mbili zinazochuana vikali kuwania ubingwa wa Ligi Kuu.

Mechi hii inatarajiwa kupigwa katika dimba la Anfield saa 1:30 usiku na utakuwa mchezo wa 11 kuzikutanisha timu hizo kwenye michuano yote tangu 2016 na Man United imeshinda mchezo mmoja tu wa mwaka 2018 tangu hapo haijawahi kupata ushindi tena ikipoteza mbili na kutoa sare mbili.

Msimu ulipita mechi yakwanza ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 na wapili Man United ilikubali kichapo cha mabao 2-0.

Tangu Aprili 28, 1894 timu hizi zimekutana mara 232 na Man United imeshinda mara 88, huku Liver ikishinda 77 na 67 zilimalizika kwa sare.

Utamu zaidi upo kwenye msimamo wa ligi ambapo Man United inaongoza ikiwa na alama 36 nyuma ya Liverpool yenye alama 33 na ikishinda itakaa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Man United imefunga mabao 34 na kufungwa 24 na Liverpool imefunga mabao 37 na kufungwa 21.

Kama Man United itashinda itafikisha alama 39 na itazidi kutengeneza pengo kubwa la alama kati yake na timu zinazomfuatia.

Liver tangu ipate ushindi wa mabao 7-0 mbele ya Crystal Palace haijapata ushindi kwenye mechi tatu zilizofuatia za EPL ikifungwa moja na kutoa sare mbili. Lakini Man United imeshinda kwenye mechi tatu mfululizo tangu ilipotoa sare ya bao 2-2 na Leicester City.

Ikiwa Liver itapoteza mechi hii, kuna uwezekano ikashuka hadi nafasi ya tano, kwani Man City ina alama 32 na imecheza mechi 16 wakati na mechi ijayo itacheza na Crystal Palace, hivyo wakishinda watafikisha alama 35.

Vile vile Everton na Leicester City zina alama 32 na michezo sawa naye hivyo kama zitashinda zitamshusha moja kwa moja.


Matokeo ya mechi za jana; Fulham 0-1 Chelsea, Leicester 2-1 Southampton, West Ham 1-0 Burnley, Leeds 0-1 Brighton, Wolves 2-3 West Brom.