Bailly avunja mtu mbavu, afungiwa mechi saba

New Content Item (1)
New Content Item (1)

MARSEILLE, UFARANSA. BEKI wa kati, Eric Bailly ameripotiwa kufungiwa mechi saba baada ya kuruga daruga la staili ya kung-fu na kumvunja mbavu mchezaji mwenzake uwanjani.

Bailly, 28, alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kufanya hivyo kwenye Kombe la Ufaransa, wakati alipomrukia daruga la kifuani mchezaji wa timu ya Daraja la Nne, Hyeres - staa, Moussa N'Diaye. Rafu hiyo ilimfanya N'Diaye kuwahishwa hospitalini kwa matibabu ya kina.

Na sasa beki huyo, ambaye yupo Marseille kwa mkopo akitokea Manchester United - atatumikia adhabu ya mechi saba kwa mujibu wa La Provence.

Staa wa Hyeres, Moussa N’Diaye alitolewa uwanjani kwa machela na kuwahishwa hospitali, huku ikielezwa alivunjika mbavu na maumibu makali kwenye mapafu na ini. Bailly alimtembelea N'Diaye alipokuwa hospitali akipatiwa matibabu.

Bailly, tayari ameshakosa mechi mbili za Ligue 1 dhidi ya Troyes na Lorient, tangu alipoonyeshwa kadi nyekundu na sasa kuna mechi nyingine tano atakosa.

Beki huyo wa kimataifa wa Ivory Coast alijiunga na Marseille kwa mkopo wa msimu mzima akitokea Man United kwenye majira ya kiangazi mwaka jana.

Marseille itamchukua jumla Bailly kama watafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na hakika amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Wafaransa hao.