Arteta bado hajakata tamaa kumnasa Williams

Muktasari:
- Nico ambaye alifanya vizuri na Hispania katika michuano ya Euro na kuisaidia kuchukua taji, amekuwa akihusishwa na timu nyingi Ulaya ikiwa ni pamoja na Barcelona.
WINGA wa Athletic Bilbao, 22 na Hispania, Nico Williams ameendelea kwa katika rada za kocha wa Arsenal, Mikel Arteta katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Nico ambaye alifanya vizuri na Hispania katika michuano ya Euro na kuisaidia kuchukua taji, amekuwa akihusishwa na timu nyingi Ulaya ikiwa ni pamoja na Barcelona.
Licha ya Arsenal kuweka ofa nono ripoti zinaeleza fundu huyu anatamani zaidi kutua Barca ambayo ilishafanya kikao na wawakilishi wake mwaka jana.
Hata hivyo, uwezekano wa kutua timu hiyo unaonekana mdogo kutokana na hali yao ya kiuchumi ambayo inawahitaji kuuza zaidi ya wachezaji wawili ili kulipa ada yake ya uhamisho na kuendana na sheria za La Liga za matumizi ya pesa.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027. Katika msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote akifunga mabao manne na kutoa asisti tano. Katika mkataba wake kuna kipengele kinachomruhusu kujiunga na timu yoyote anayoitaka ambayo itakuwa tayari kulipa Euro 58 milioni.
Marcus Rashford
KUNA asllimia nyingi mshambuliaji wa Mancheter United, Marcus Rashford aliyejiunga na Aston Villa kwa mkopo dirisha lililopita akasaini mkataba wa kudumu wa kuendelea kuitumikia Villa au akajiunga na timu nyingine baada ya msimu kumalizika. Rashford mwenye umri wa miaka 27, alifikia hatua ya kuondoka baada ya kuondolewa katika kikosi na kocha Ruben Amorim ambaye hakufurahishwa na kiwango chake.
Justin Kluivert
NEWCASTLE United imepanga kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth na Uholanzi, Justin Kluivert, 25, katika dirisha lijalo ikiwa itamuuza Mswedeni Alexander Isak, 25. Licha ya kuwa na mkataba hadi 2028, Newcastle ipo tayari kumuachia Isak ikiwa itapokea ofa nzuri jambo ambalo linaonekana kuwa na asilimia nyingi za kutokea mwisho wa msimu kwani vigogo wengi wanahitaji huduma yake.
Alejandro Garnacho
KOCHA wa Napoli, Antonio Conte ameingia katika sintofahamu na mabosi wa timu hiyo baada ya kushindwa kusajili mastaa aliowapendekeza dirisha lililopita. Kwa mujibu wa Sky Sports, Conte alihitaji saini ya mmoja kati ya winga wa Man United na Argentina, Alejandro Garnacho, 20, na mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi, 23 ili kuziba pengo la Khvicha Kvaratskhelia aliyeuzwa PSG.
Marc Guehi
NEWCASTLE United na Tottenham Hotspur bado zina mpango wa kupigana vikumbo katika dirisha la majira ya kiangazi lijalo ili kuipata huduma ya beki kisiki wa Crystal Palace na England, Marc Guehi, 24. Kwa mujibu wa Sky Sports, Spurs ilituma ofa katika dakika za mwisho za dirisha lililopita ili kuipata saini ya nyota huyu, lakini ilikataliwa.
Gregor Kobel
CHELSEA imepanga kuanza tena mazungumzo na Borussia Dortmund dirisha lijalo la majira ya kiangaI ili kuipata saini ya kipa wa timu hiyo na Uswisi, Gregor Kobel, 27, baada ya kipa Robert Sanchez kuonyesha kiwango kibovu kwenye mechi kadhaa zilizopita. Awali, Chelsea ilikuwa ikipambana ili kumsajili katika dirisha lililopita lakini dili linadaiwa kukwama kwa sababu Dortmund haikutaka kumuuza.
Benjamin Sesko
ARSENAL imewaweka kiporo mastaa wawili ambao itawasajili dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu. Mastaa hao ni mshambuliaji wa RB Leipzig na Slovenia, Benjamin Sesko, 21 (pichani) na kiungo wa Real Sociedad na Hispania, Martin Zubimendi, 26. Sesko na Zubimendi ni miongoni mwa mastaa wanaowindwa sana.
Christopher Nkunku
MANCHESTER United na Bayern Munich zinasubiri hadi dirisha lijalo la majira ya kiangazi kabla ya kuamua kurudi tena mezani kuzungumza na Chelsea ili kuipata saini ya mshambuliaji wa timu hiyo na Ufaransa, Christopher Nkunku, 27, baada ya kufeli dirisha lililopita. Moja kati ya sababu zinazodaiwa kukwamisha ni Chelsea kuhitaji kiasi kikubwa cha pesa.