Arteta apata wa kumrithi Lacazette

Wednesday October 06 2021
arteta pic

LONDON, ENGLAND. ARSENAL tayari imeshaanza kuwatambua mastraika ambao itahitaji kunasa saini zao ikiwa ni maandalizi ya kuachana na supastaa wao, Alexandre Lacazette.

Mastaa wa kimataifa wa England, Dominic Calvert-Lewin wa Everton na Ollie Watkins wa Aston Villa wanatajwa kuwapo kwenye orodha ya wachezaji wanaosakwa na Arsenal kwenda kuchukua mikoba ya Lacazette.

Lacazette, 30, yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake wenye thamani ya Pauni 180,000 kwa wiki na hajapewa ofa yoyote ya mkataba mpya.

Kuna uwezekano mkubwa wa Arsenal ikafungua milango ya kumpiga bei kwenye dirisha la uhamisho wa Januari, wakiepuka kumpoteza bure kabisa mwishoni mwa msimu. Lakini, kocha Mikel Arteta ataruhusu hilo kutokea kama tu ataweza kusaini mshambuliaji mwingine wa kusaidiana na Pierre-Emerick Aubameyang.

Baada ya kutumia Pauni 148 milioni kusajili wachezaji sita kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, Arsenal wamepanga kufanya usajili mwingine Januari mwakani.

Lacazette, aliyenaswa kwa Pauni 52 milioni akitokea Lyon mwaka 2017, hajaanzishwa kwenye mechi yoyote ya Ligi Kuu England msimu huu baada ya kupata maambukizi ya Uviko 19 siku moja kabla ya kuanza kwa msimu huu.

Advertisement

Kwenye kikosi cha Arsenal, yeye ndiye mshambuliaji pekee mwenye uzoefu ukimweka kando Aubameyang, hivyo kama ataondoka ataacha pengo ambalo Arteta atakuwa na shughuli la kubwa ya kuliziba.

Hata hivyo, washambuliaji Calvert-Lewin, 24, na Watkins, 25, ambao Arteta anawataka wote wapo na mikataba mirefu kwenye timu zao, itakayofika tamati 2025, hivyo saini zao haziwezi kupatikana kwa gharama nafuu.

Advertisement