Arsenal yawafungia kazi Jesus, Raphinha

Arsenal yawafungia kazi Jesus, Raphinha

Muktasari:

  • Arsenal imepanga kuhakikisha usajili wa washambuliaji wawili wa Brazil, Gabriel Jesus na Raphinha unakamilika wiki hii kabla ya kugeukia nyota wengine kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao.

London,England. Arsenal imepanga kuhakikisha usajili wa washambuliaji wawili wa Brazil, Gabriel Jesus na Raphinha unakamilika wiki hii kabla ya kugeukia nyota wengine kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao.

Baada ya ofa ya kwanza ya Pauni 35milioni (Sh100 bilioni) kwenda kwa Manchester City kwa ajili ya Jesus kukataliwa, Arsenal imeamua kurudi upya katika meza ya mazungumzo na sasa imepanga kutumia upande wa mchezaji huyo kulazimisha uhamisho.

Imeripotiwa kuwa wakala wa Jesus, Marcelo Pettinati amelazimika kusafiri hadi England mwishoni mwa wiki iliyopita ili kukutana na uongozi wa Manchester City kuwaomba wamuachie nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 ajiunge na Arsenal.

Arsenal inaamini itakuwa rahisi kwao kumnyakua Jesus ikiwa upande wa mshambuliaji huyo utalazimisha uhamisho kwani hilo litaifanya Manchester City kupunguza dau la uhamisho kwa nyota huyo wa Brazil tofauti na lile la Pauni 50milioni (Sh143 bilioni) ambalo wanahitaji kwa sasa ili kumruhusu Jesus aondoke.

Baada ya kuitumikia Manchester City kwa miaka mitano, Jesus ameonekana kuwa na hamu ya kusaka timu ambayo itampatia nafasi ya kutosha ya kucheza na anaipa Arsenal kipaumbele cha kwanza kutokana na timu hiyo kutokuwa na mshambuliaji wa daraja la juu kulinganishwa na yeye.

Kingine kinachoonekana kumpa Jesus hamu ya kujiunga na Arsenal ni uwepo wa kocha Mikel Arteta ambaye aliwahi kufanya naye kazi katika kikosi cha Manchester City,
miaka michache iliyopita pindi alipokuwa msaidizi wa Pep Guardiola.

Mbali na Arteta, Jesus pia anavutiwa na uwepo wa kundi kubwa la raia wenzake wa Brazil katika kikosi hicho cha Arsenal wakiongozwa na mkurugenzi wa ufundi, Edu Gaspar huku upande wa wachezaji wakiwepo Gabriel Martinelli, Gabriel Magalhaes na Marquinhos aliyenunuliwa hivi karibuni kutokea Sao Paulo.

Jesus ameichezea Manchester City jumla ya michezo 236 tangu alipojiunga nayo mwaka 2016 akitokea Palmeiras ya Brazil ambapo katika idadi hiyo ya michezo, amehusika na jumla ya mabao 141, akifunga mara 95 na kupiga pasi za mwisho 46.

Wakati ikipambania usajili wa Jesus, Arsenal pia ipo katika hatua nzuri ya kumnasa winga wa Leeds United ambaye pia ni Mbrazil, Raphinha baada ya kufanya mazungumzo na wakala wa mchezaji huyo ambaye ni nyota wa zamani wa Ureno na Barcelona, Deco.

Arsenal inatajwa kuwa ipo tayari kutoa kitita cha Pauni 60milioni (Sh172 bilioni) ambacho Leeds United imepanga kama bei ya kumuuza nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 ambaye anamudu vyema kucheza nafasi zote za winga.

Awali kipaumbele cha Raphinha kilikuwa ni kujiunga na Barcelona lakini miamba hiyo ya Hispania inaonekana kutokuwa tayari kutoa kiasi hicho cha Pauni 60milioni na inaelekea kujitoa katika mbio za kumuwania nyota huyo.

Raphinha alikuwa nyota tegemeo wa Leeds United katika msimu uliomalizika ambao aliibuka mfungaji bora wa klabu hiyo akifumania nyavu mara 11 katika jumla ya mechi 35 za Ligi Kuu ya England huku akipiga pasi za mwisho tatu.

Mbali na Raphinha na Jesus, Arsenal pia imapanga kufanya usajili wa kiungo wa Leeds United, Kalvin Phillips na beki wa kati ya Brighton, Marc Cucurella.