Arsenal yavunja rekodi

LEICESTER, ENGLAND

BAADA ya kuichakaza Leicester City mabao 3-1, Arsenal imeweka rekodi ya kushinda mechi ya ugenini dhidi ya timu zilizo kwenye nafasi tatu za juu za Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu Januari, 2015 ilipoinyuka Manchester City mabao 2-0.

Tangu hapo ilicheza mechi 14 dhidi ya timu za nafasi hizo bila kupata ushindi ikitoka sare mara tatu na kukubali kufungwa mara 11.

Arsenal ilijipatia bao la kwanza kupitia David Luiz  aliyefunga dakika ya 39 kwa kichwa kikali baada ya mpira uliopigwa na Willian.

Alexandre Lacazette akafunga bao la pili kwa njia ya penalti dakika za nyongeza kipindi hicho cha kwanza na akaweka rekodi ya kufunga penalti zote tano alizoipigia timu hiyo kwa msimu ambapo anashika nafasi ya pili kwa utupiaji wa mabao kwenye kikosi cha Arsenal namba moja akiwa ni  Pierre-Emerick Aubameyang mwenye 13 huku yeye akiwa na 11.

Katika dakika ya 52 kipindi cha pili mwamba Nicolas Pepe aliiandikia Arsenal bao la tatu ambalo kwake ni  la nne kwenye mechi saba za mwisho.

Leicester ndio ilikua ya kwanza kupata bao dakika ya sita kipindi cha kwanza kupitia Youri Tielemans.

Arsenal inashika nafasi ya 10 ikiwa na alama 37 baada ya kucheza mechi 26, wakati Leicester imeendelea kusalia nafasi ya tatu kwa alama 49 baada ya kucheza mechi 26.