Zidane atema povu Laliga

PAMPLONA. HISPANIA. WAMEZINGUA. Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amechukizwa na uamuzi wa chama cha soka nchini Hispania kuwalazimisha kucheza mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Osasuna licha ya uwepo wa barafu za kutosha katika dimba la El Sadar Stadium lililopo huko Jijini Pamplona.

Hiki ni kipindi cha baridi barani Ulaya na maeneo mengi yamegubikwa na barafu ambazo zimekuwa nyingi hadi kusababisha kuahirishwa kwa baadhi ya mechi ikiwa ni pamoja na ile ya Atletico Madrid na Athletic Bilbao Jumamosi iliyopita.

Madrid ililazimika kusafiri hadi Pamplona ili kucheza mechi hiyo licha ya hali mbaya ya hewa iliyochagizwa na barafu zilizochelewesha ndege yao kwa saa mbili ili kupisha wafanya usafi watoe barafu zilizojaa kwenye barabara za uwanja wa ndege wa Madrid.

Ulikuwa ni mchezo ambao timu zote mbili hazikupata nafasi ya kucheza soka vizuri na kuzifanyia kazi mbinu za makocha na mwisho ukamalizika kwa suluhu.

“Tulifanya tulichotakiwa tufanye uwanjani lakini haukuwa mchezo wa mpira wa miguu, hali ilikuwa tofauti na mbaya sana,” alisema.

Hali hiyo ya hewa imesababisha usafiri wa anga kutoka Pamplona walipocheza mechi hadi Madrid kusitishwa, hivyo hawakuweza kuondoka na wanaangalia uwezekano wa kuondoka leo Jumatatu.

“Mambo yaliyotokea kwenye siku hizi mbili yanachanganya sana na hatujui hata lini tunaweza kurejea Madird,

“Huu mchezo ilibidi usimamashwe na hilo lipo wazi kwa sababu mazingira ya kuchezea mechi hayakuwa yamekidhi vigezo,” alisema Zidane na alipulizwa kuhusiana na chama cha soka nchini humo ambacho ndio kimeruhusu mechi nyingi kuchezwa wikiendi hii alisema hawezi kuingilia uamuzi wao, yeye na timu yake wamefanya kile ambacho wameagizwa kufanya na wamemaliza.

“Mbaya zaidi sijui nitarudi lini Madrid Jumatatu au Jumanne na ukumbuke Jumatano tuna mchezo mwingine.”