Zidane apewa mechi 4 tu

Zidane apewa mechi 4 tu

MADRID, HISPANIA. MAMBO ni moto. Zinedine Zidane ameripotiwa kwamba, ana mechi nne tu za kuamua hatima ya kibarua chake huko Real Madrid huku mabosi wake wakianza kumtolea macho Mauricio Pochettino kwenda kuchukua mikoba yake fasta.

Real Madrid ilikumbana na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Shakhtar Donetsk kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi na hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kuangukia katika Europa League.

Kichapo hicho kimefuatia kile cha Alaves kwenye La Liga wikiendi iliyopita, kilichowafanya wakamate nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, pointi saba nyuma ya vinara Real Sociedad.

Na kwa mujibu wa Marca, Zidane sasa ana mechi nne tu za kuokoa kibarua chake huku Pochettino akikaa mkao wa kuwa tayari kwenda kunyakua ajira hiyo huko Bernabeu

Hiki ni kipindi kigumu zaidi kwa kocha Zidane kwa sababu hizo nne, atacheza dhidi ya Sevilla, Borussia Monchengladbach, mahasimu wao Atletico Madrid na wababe wengine wa La Liga, Athletic Bilbao.

Zidane, ambaye aliongoza miamba hiyo ya Bernabeu kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo katika awam yake ya kwanza ya ajira huko Los Blancos, alisisitiwa kwamba hajiuzulu.

Baada ya matokeo ya mechi ya Shakhtar, Zidane alisema: “Sijiuzulu, sina huo mpango. Siku zote ni kawaida kuwa na nyakati kama hizi. Ni kweli kabisa hiki ni kitu kibaya kutokana na matokeo, lakini ni lazima tuendelee. Ni nyakati ngumu, lakini naamini tutarudi kwenye ubora wetu. Tutashinda mechi inayofuata. Nina uhakika tutafanya hivyo.”

Lakini, uamuzi wa mwisho si wa kwake, huku mabosi wake tayari wakianza kupiga hesabu za kumchukua Muargentina, Pochettino akachukue mikoba yake. Na tayari imeshaanza kujadiliwa namna kikosi cha Pochettino kitakavyokuwa huko Real Madrid, ikidaiwa kwamba bila ya shaka atahitaji Harry Kane na Dele Alli watue kwenye timu yake sambamba na Paulo Dybala. Zidane amewahi kuipa Real Madrid mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa.