Ronaldo aifikia rekodi ya Messi Ulaya

Ronaldo aifikia rekodi ya Messi Ulaya

Muktasari:

Kiujumla Ronaldo amepachika mabao 131 kwenye michezo 172 aliyocheza mpaka sasa kwenye Ligi hiyo ya Mabingwa Ulaya.


TURIN, ITALIA. BAO alilofunga mshambuliaji wa Juventus, Cristiano Ronaldo kipindi cha  kwanza kwenye mchezo wa jana Jumanne wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya  Ferencvaros limemfanya kuifikia rekodi ya mpinzani wake mkubwa Lionel Messi.

Ronaldo ambaye ameisaidia Juve kufuzu hatua ya mtoano baada ya kuisadiia kupata ushindi wa mabao 2-1, ameifikia rekodi ya Supastaa wa Barcelona, Messi kwa kufunga mabao 70 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya huku akiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Juve katika mchezo huo ndio ilianza kutanguliwa kufungwa dakika ya 19 kwa bao la Myrto Uzuni kabla ya Ronaldo kusawazisha dakika 35 na Alvaro Morata kuifungia timu yake bao la ushindi dakika ya 90+2.
 
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Ronaldo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu  apone maambukizi ya virusi vya corona na bao alilofunga kwenye mchezo huo ni la kwanza kwake katika michuano hiyo msimu huu.

Mbali na Juve ambayo imetinga hatua hiyo ya mtoano licha ya kwamba zimebaki mechi mbili kabla ya hatua ya makundi kumalizika, klabu nyingine ambazo tayari zimejikatia tiketi ni Barcelona, Chelsea na Sevilla.

MATOKEO KAMILI

Krasnodar 1 -  2 Sevilla
Rennes 1-2 Chelsea
Dortmund 3 -  0 Club Brugge KV
Dyn. Kyiv 0- 4 Barcelona
Juventus 2- 1 Ferencvaros
Lazio 3- 1 Zenit
Manchester Utd 4 -  1 Basaksehir
PSG 1 - 0 RB Leipzig