Msikie Bruno kuhusu Man Utd

Msikie Bruno kuhusu Man Utd

MANCHESTER, ENGLAND. MAJANGA. Bruno Fernandes amewachana wachezaji waenzake kuwa hawastahili kuvaa jezi ya Manchester United, baada ya kipigoncha kushtukiza cha mabao 4-0 walichopata dhidi ya Brighton kwenye mchezo wa Ligi Kuu England wikiendi iliyopita.

Mreno huyo aliumizwa na kiwango kibovu walichoonyesha kwenye mchezo huo uliyochezwa uwanja wa Amex nje kidogo ya jiji la Manchester na kushangaza mshabiki.

Man United imepoteza nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza ligi ikiwa imejikita katika nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa imebakiwa na mchezo mmoja.

Aidha, kauli ya Bruno ameithibitisha baada ya mashabiki wa Man United kutamka wazi kwamba wachezaji hawafiti kukipiga katika timu hiyo kutokana na uwezo wao mdogo uwanjani. Akizungumza baada ya mchezo huo kuisha kupitia kituo cha televisheni cha Sky Sports Bruno alisema hata yeye hastahili kuvaa jezi ya Man United.

“Kilichotokea leo ni kweli hatustahili kuvaa jezi ya Man United, nimekubali na mashabiki wana haki ya kutuponda, matokeo ni mabaya, Brighton walikuwa bora zaidi yetu, na walistahili kupata ushindi,” alisema Bruno.

Naye kocha wa mpito Ralf Rangnick anayemaliza muda wake aliomba radhi mashabiki kwa kipigo hicho cha kudhalilisha uwanja wa Amex.

“Ni kiwango kibovu sana vijana wameonyesha, kuanzia kipindi cha kwanza hadi kipenga cha mwisho, niwaombe radhi mashabiki kwa matokeo hayo,”alisema Rangnick.