Inter,Madrid vitani Uefa leo

Inter,Madrid vitani Uefa leo

Muktasari:

Baada ya hatua hiyo kumalizika, hatua inayofuata ni ile ya 16 bora ambapo timu mbili kwa kila kundi zitafuzu na ile ya tatu itakwenda kushiriki hatua ya 32 bora ya michuano ya Europa League.

MILAN, ITALIA. Hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inatarajiwa kuendelea leo ambapo mchezo wa kukata na shoka utakuwa kati ya Inter Milan na Real Madrid ambazo zote zinapambana kufuzu katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.
Timu hizo zilizopangwa kwenye kundi B, zitakuwa zinacheza mchezo wa nne kwenye hatua hiyo, lakini zinaingia zikiwa kwenye hali mbaya ya kuwa timu mbili zinazoshika nafasi mbili za mwisho katika kundi hilo lenye timu nne.
Madrid inashikilia nafasi ya tatu ikiwa na pointi nne baada ya kucheza mechi tatu ambapo imepoteza moja, sare moja na kushinda moja huku mpinzani wake Inter Milan ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi mbili baada ya kucheza mechi tatu ikitoa sare mbili na kupoteza moja.
Hata hivyo mbali ya mechi hiyo itakayopigwa saa 5:00 usiku mchezo mwingine kwenye kundi hilo utakuwa kati ya Borussia Moenchengladbach dhidi ya Shakhtar Donetsk utakaopigwa saa 2:55 usiku.
Katika Kundi A, Atletico Madrid inayoshika nafasi ya pili itakuwa na kibarua mbele ya Lokomotiv Moscow katika mchezo utakaoanza saa 5:00 usiku na Bayern Munich inayoshikilia nafasi ya kwanza itaikaribisha Salzburg.
Olympiacos ya kundi C itaumana na Manchester City ambao ndio vinara wa kundi hilo wakiwa wameshinda mechi zote tatu za kwanza. Mechi hiyo itaanza saa 2:55 usiku na mchezo mwingine wa kundi hilo utakuwa kati ya Marseille na FC Porto ukaopigwa saa 5:00 usiku.
Ajax iliyopo kundi D itajipima ubavu na FC Midtjylland katika mchezo utakaopigwa saa 5:00 usiku kabla ya Liverpool kufunga dimba kwa kuikabili Atalanta.