Ile michuano ya Super League Ulaya inarudi kivingine

LONDON, ENGLAND. WATU hawashindwi. Licha ya mashabiki kuandamana na vurugu kutawala kwenye mitaa ya nchi mbalimbali barani Ulaya kufuatia wazo la European Super League, jamaa hawajakata tamaa na wameamua kuliamsha tena.

Unaambiwa Super League ipo njiani kurejea lakini safari hii kutakuwa na maboresho kibao ikiwa pamoja na hadi mashabiki kupewa pesa ili kwenda kutazama mechi za ugenini.

Aprili mwaka huu, timu 15 barani Ulaya ikiwa pamoja na timu sita kutoka Ligi Kuu England ambazo ni Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham zilikubaliana kuanzisha ligi yao jambo lililozua mtafaruku mkubwa kwa mashabiki waliokuwa wanaonekana kupinga suala hilo.

Baada ya vurugu, timu zote za Ligi Kuu England ziliamua kujitoa kwenye mpango huo na kuziacha Real Madrid, Barcelona na Juventus zikiwa bao na matumaini ya kuwa na ligi hiyo.

Baada ya kufikiria kwa muda mrefu vigogo waliokuja na wazo hilo ambao ni mabosi wa timu zote 15 wameamua kuja na maboresho ambayo wanaamini yatawafanya mashabiki na mabosi wa Uefa kutopinga wazo lao, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Mpango huo mpya unaeleza kwamba kutakuwa na ligi mbili ambapo kila ligi itajumuisha timu 20, hivyo kutakuwa na idadi ya timu 40 ambazo zitashiriki kila msimu.

Vilevile kutakuwa na kupanda na kushuka kwa timu zitakazoshiriki na timu yoyote inayocheza kwenye ligi moja wapo barani Ulaya itakuwa na nafasi ya kushiriki michuano hiyo ikiwa itafanya vizuri kwenye ligi ya ndani.

Uwepo wa kupanda na kushuka umezingatia kwamba ligi hiyo isiwe ya timu maalumu na badala yake timu nyingi zipate nafasi.

Mbali ya hilo, mpango huo mpya umelenga kuwapoza mashabiki na kuwateka kihisia kwani watakuwa wanapewa msaada wa pesa kwa ajili ya kwenda kutazama mechi za ugenini.

Pia kutakuwa na viingilio vya chini kwa nusu ya uwanja mzima ili kuwapa nafasi mashabiki ambao hawana uwezo mdogo kiuchumi kupata burudani.

Super League ni miongoni mwa mashindano yatakayozifaidisha klabu husika ikiwa yataanzishwa kwani timu zitakazoshiriki tu, zitakuwa na uhakika wa kupata Pauni 4.6 bilioni kama pesa ya awali.

Hii imesababisha wamiliki na waandaaji wa michuano hiyo kusisitiza kwamba lengo lao ni kuzifanya timu ziishi kulingana na kile zinachokiingiza kama sheria za Uefa zinavyoeleza.

Mpango huo mpya umekuja siku chache baada ya serikali ya Hispania kutoa tamko kwamba hawaungi mkono uanzishwaji wa ligi hiyo na watapambana na wapanga-njama wanaodhamiria kuianzisha.

Mpango wa Super League uliibuka mapema mwaka huu, katika kipindi ambacho timu nyingi kubwa barani Ulaya zilikuwa zikikumbana na ukata wa kipesa baada ya uchumi kuyumba kutokana na athari za janga la Uviko 19.