Hazard aende PSG, Mbappe aje Madrid

Hazard aende PSG, Mbappe aje Madrid

PARIS, UFARANSA. HABARI ndo hiyo. Lisemwalo ni kwamba Real Madrid wamepanga kumtumia Eden Hazard kama chambo cha kumnasa staa wao wanayemfukuzia muda mrefu, Kylian Mbappe.

Hazard amekuwa na wakati mgumu tangu atue Madrid akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara huku saini yake iligharimu pesa nyingi kutoka Chelsea kwa ada ya Pauni 130 milioni Juni 2019.

Na sasa, kwa mujibu wa kipindi cha televisheni huko Hispania cha El Chiringuito, Los Blancos sasa wanajiandaa kuachana na staa huyo wa Kibelgiji.

Tumaini lao ni kuwa Hazard anaweza kutumika kuwalainisha PSG kumwaachia Mbappe kwenda kujiunga na miamba hiyo ya La Liga.

Hazard atakuwa nje ya uwanja hadi Mwaka Mpya baada ya kuumia misuli kwenye mchezo wa kipigo dhidi ya Alaves.

Sambamba na hilo, Hazard alitumika pia kwa siku 392 bila ya kufunga kwenye kikosi cha Zinedine Zidane.

Kwa miaka miwili sasa, Mbappe amekuwa kwenye rada za Real Madrid na mkataba wake huko Paris utafika tamati mwishoni mwa msimu wa 2021-22 na hakuna dalili zozote za kusaini dili jipya huko PSG. Mbappe aliwahi kusema hivi: “Unapokuwa kijana na Mfaransa, shujaa wako ni Zidane.”

Na Zidane alisema: “Kama mnavyofahamu, nimekuwa nikimfahamu Mbappe kwa muda mrefu. Nampenda sana, kwanza kama mtu, kwa sababu alikuja kufanya majaribio hapa huko nyuma.” Kwa sasa kinachosubiriwa ni muda huo mchakato uanze.