Giroud aweka rekodi Ligi ya Mabingwa

Giroud aweka rekodi Ligi ya Mabingwa

London, England. Olivier Giroud ameweka rekodi mpya Ulaya baada ya kufunga mabao manne dhidi ya Sevilla, lakini alikiri kuwa anaweza kuanzia benchi pia katika mchezo wa kesho.

Giroud alipewa heshima na benchi zima la Chelsea kwa kusimama wakati akitoka uwanjani baada ya kufunga mabao manne na kuwa mcchezaji wa kwanza mwenye umri mkubwa kufunga ‘hat-trick’ katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Akiwa na miaka 34, mshambuliaji huyo bado hafahamu kama amefanya makubwa kiasi cha kupewa nafasi ya kuanza kwenye mchezo wa kesho wa Ligi Kuu England, wakati Blues itakapoivaa Leeds.

Giroud alisema baada ya mchezo huo: “Niacheni tu nifurahie usiku wangu, huu ni ushindi mkubwa. Baada ya kupumzika ndiyo nitajua mipango ya mchezo ujao itakuwaje.”

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alikiri kuwa mwezi uliopita angelazimika kuondoka Stamford Bridge kama asingepewa wakati wa kucheza.

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Sevilla ulikuwa wa pili kwake kuanza katika kikosi cha Chelsea msimu huu, lakini Kocha wa Blues, Frank Lampard amekiri kuwa itakuwa ngumu kwake kumwacha mkongwe huyo katika mchezo wa kesho.

Lampard alisema: “Tutaona itakavyokuwa, ni uamuzi mgumu lakini amefunga mabao manne katika mechi moja.”