Eti Klopp atambeba kiulaini tu Koulibaly

Eti Klopp atambeba kiulaini tu Koulibaly

LIVERPOOL ENGLAND. STAA wa zamani wa Liverpool, John Barnes anaamini Jurgen Klopp anaweza kumshawishi Kalidou Koulibaly na kumnasa kirahisi tu kwenye dirisha la Januari.

Barnes anaamini beki huyo wa kati wa Napoli hatapuuzia nafasi ya kwenda kucheza sambamba na Mdachi Virgil van Dijk kama Klopp atafungua milango ya kunasa huduma yake.

Lakini, kama Koulibaly hatapatikana kwenye dirisha la Januari, Barnes alisema kwamba Liverpool hawatapaswa kufanya usajili wa beki mwingine kwa sababu haoni ni mchezaji gani mwingine atakuja kuboresha kikosi hicho cha Anfield.

Koulibaly na wachezaji wengine wa Napoli wanaaminika kwamba, hawajalipwa tangu Julai baada ya miamba hiyo ya Italia kukumbwa na ukata wa kiuchumi. Kutokana na hilo, mastaa hao wanaweza kupatikana kwa gharama nafuu katika dirisha lijalo.

Na Koulibaly ni staa mwenye jina kubwa zaidi katika kikosi hicho baada ya kujitengenezea sifa ya kuwa mmoja wa mabeki wa kati bora kabisa Ulaya.

Chelsea, Manchester United na Manchester City sambamba na PSG ni vigogo wengine wa Ulaya wanatajwa kufukuzia huduma yake.