Chelsea ubingwa ndiyo basi tena

LONDON ENGLAND.  KOCHA wa Chelsea, Thomas Tuchel, amechukizwa na sare ya bao 1-1 waliyopata dakika za mwisho walipoumana na Brighton usiku wa kuamkia jana, na amefuta ndoto zao katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Tuchel aliwaka baada ya mtanange huo ulipomalizika akisisitiza nafasi ya Chelsea ya kuwania ubingwa msimu huu ni ndogo sana na watakuwa na safari ndefu ya kuifukuzia Manchester City yenye pointi 50, kwenye msimamo baada ya kuifunga Brentford.

Baada ya Chelsea kudondosha pointi mbili dhidi ya Brighton, Tuchel ameweka wazi timu yake ina lundo ya wachezaji majeruhi ambao ni tegemeo akiwemo Reece James, aliyeumia katika kipindi cha kwanza cha mtananage huo.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Tuchel alisema hawajapata taarifa kuhusu hali ya James.

“Nadhani ameumia misuli ya paja. Kuelekea mechi ya Liverpool itakuwa ngumu sana, sasa tuna kazi ya kutafuta mchezaji mwingine wa kuziba pengo, kila mtu ameumia, wengine wanarejea baada ya kuugua corona, tuna wachezaji wachache, ni upuuzi kudhani kwamba bado tumo kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa. Kila timu ina wachezaji wake muhimu na wapo fiti itakuwa upuuzi mtu akifikiria hivyo,” alisema Tuchel.

Chelsea ilipata ahueni baada ya Romelu Lukaku kurejea na kufunga bao katika mechi ya Ligi Kuu England, Chelsea ilipoilaza Norwich City mabao 3-1.

Baada ya straika Danny Welbeck kufunga bao la dakika za lalasalama na kuipa Brighton sare ya 1-1, Tuchel alisema kila kitu hakiwaendei vyema kwani refa aliwanyima penalti wakati wakiongoza 1-0.