Busquets, Pique panga linawahusu

Busquets, Pique panga linawahusu

BARCELONA HISPANIA. KIUNGO mkata umeme, Sergio Busquets huenda akawa kwenye orodha ya mastaa ambao Barcelona itawapiga chini kwenye kikosi chao kwa kuwa mishahara yao ni mikubwa na klabu ina hali mbaya ya uchumi.

Barcelona wanataka kuweka sawa mambo yake ya pesa wakipanga kuwapiga chini mastaa watatu ambao wamekuwa na mishahara mikubwa kwenye kikosi hicho cha Nou Camp. Mastaa wengine waliopo kwenye hatari ni mabeki Jordi Alba na Gerard Pique.

Kwa mujibu wa Sport, mabosi wa Barcelona wanataka kupunguza bili yao ya mishahara kwa Pauni 150 milioni.

Kwa sasa bili ya mishahara ya miamba hiyo ya Nou Camp ni Pauni 546 milioni, lakini kiwango ambacho wanapaswa kulipa ni kati ya Pauni 376 milioni na Pauni 402 milioni. Mastaa hao watatu ambao wote ni manahodha wa Barca, wanalipwa mishahara mikubwa, lakini wakati Busquets akiwa bado muhimu kwenye kikosi, Alba na Pique wao wamekuwa wakitupwa kando.

Mastaa hao wamecheza zaidi ya mechi 1,700 na wamebeba mataji kibao kwenye kikosi hicho, lakini kwa sasa timu ikiwa chini ya Xavi, siku zao zinahesabika huko Nou Camp. Wakati wa dirisha lililopita, Barca ilitumia Pauni 145 milioni, ambayo iliwawezesha kuwanasa mastaa matata kabisa kama Robert Lewandowski, Jules Kounde na Raphinha.