Auba atema cheche, UEFA imerudi

Auba atema cheche, UEFA imerudi

LONDON ENGLAND. STRAIKA, Pierre-Emerick Aubameyang amechimba mkwara na kusema atatumia maujuzi na mbinu alizochota kwa Ronaldo orijino ili kuibeba Chelsea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya watakapoivaa AC Milan uwanjani Stamford Bridge kesho, Jumatano.

The Blues haijashinda mechi yoyote kati ya mbili ilizocheza kwenye kundi lake msimu huu na inashika mkia Kundi E.

Aubameyang, ambaye alianza maisha yake ya soka Milan, alifungua akaunti yake ya mabao Chelsea wakati alipofunga bao la kusawazisha dhidi ya Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England, Jumamosi.

Akiwa Milan, Auba hakucheza mechi yoyote kwenye kikosi cha kwanza, lakini alikuwa akifanya mazoezi na Ronaldo wa Brazil, huku mkali huyo wa Gabon akidai kwamba amechota ujuzi mwingi sana kutoka kwa gwiji huyo wa soka duniani.

Aubameyang alisema: “Timu ile ilikuwa kubwa sana kusema ukweli. Ronaldo, Paolo Maldini, Alessandro Nesta - na kipindi kile nilikuwa mdogo sana.”

Mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya unarejea wiki hii, ambapo leo Jumanne na kesho Jumatano kutakuwa na shughuli pevu viwanjani ambapo kila timu itashusha karata yake ya tatu kwenye hatua ya makundi.

Leo, Ajax itakipiga na Napoli na Liverpool watamalizana na Rangers kwenye Kundi A, wakati Club Brugge itaikabili Atletico Madrid huku FC Porto wakimalizana na Bayern Leverkusen kwenye Kundi B. Bayern Munich watacheza na Viktoria Plzen na Inter Milan watakipiga na Barcelona kwenye Kundi C, huku Marseille wakicheza na Sporting CP na Eintracht Frankfurt watakipiga na Tottenham Hotspur katika mechi za Kundi D.

Kesho, Chelsea na Milan wakati RB Salzburg watacheza na Dinamo Zagreb kwenye Kunsi E, wakati RB Leipzig ikikipiga na Celtic na Real Madrid wakimaliza utata na Shakhtar Donetsk kwenye Kundi F, huku Kundi G litashuhudiwa wababe Manchester City wakicheza na FC Copenhagen na Sevilla watakipiga na Borussia Dortmund. Kundi H litashuhudiwa wababe, Benfica wakicheza na Paris Saint-Germain na Juventus watakipiga na Maccabi Haifa.