Amsha dude! Moto ni mkubwa usiku wa Mabingwa Ulaya

LONDON, ENGLAND. NI mwendo wa kuamsha dude. Ndicho unachoweza kusema kuhusu kurejea kwa mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Shughuli ni pevu. Vita inaanza usiku wa leo Jumanne na kesho Jumatano. Visasi na rekodi zinasakwa.

Barcelona wamepewa nafasi ya kulipa kiasi dhidi ya Bayern Munich, wakikumbuka mechi waliyochapwa Bao Nane huko nyuma. Lakini, safari hii Barca haitakuwa na huduma ya Lionel Messi wala Antoine Griezmann na tumaini lao litakuwa kwa Memphis Depay katika kukabiliana na chama hilo la Robert Lewandowski.

Hiyo ni mechi ya kwanza katika Kundi E, huku mechi nyingine kwenye kundi hilo Dynamo Kiev watakipiga na Benfica.

Mambo ni moto, supastaa Cristiano Ronaldo na chama lake la Manchester United lenye wakali kibao akiwamo Paul Pogba, Bruno Fernandes na Jadon Sancho watakuwa ugenini kukipiga na Young Boys katika mechi ya Kundi F, huku kutakuwa na mchakamchaka mwingine kwenye kundi hilo, wakati mabingwa wa Europa League, Villarreal watakapokipiga na Atalanta.

Straika Romelu Lukaku baada ya kurejea Stamford Bridge ataiongoza Chelsea dhidi ya Zenit St. Petersburg katika Kundi H. Chelsea ya kocha Thomas Tuchel itaanza kampeni kutetea ubingwa wa michuano hiyo nyumbani, huku mechi nyingine kwenye kundi lao, Malmo FF itacheza na Juventus.

Mchezo wa mwisho wa kwa usiku wa leo, Sevilla itakipiga na FC Salzburg na mabingwa wa Ufaransa, Lille watacheza na Wolfsburg.

Supastaa Lionel Messi ataonekana Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa ndani ya jezi isiyokuwa ya Barcelona, wakati chama lake jipya, Paris Saint-Germain litakapokwenda ugenini kukipiga na Club Brugge kesho Jumatano. Miamba hiyo imepangwa Kundi A, huku mashabiki wakisubiri kuona itakachofanya kwenye michuano hiyo kwa kuwa na kikosi chenye safu hatari ya ushambuliaji inayoundwa na Kylian Mbappe na Neymar.

Mechi nyingine kwenye kundi hilo linalotajwa kuwa ni la kifo, itakutanisha chama la Pep Guardiola Manchester City lenye wakali kama Kevin De Bruyne, Jack Grealish, Raheem Sterling kwa kuwatazama kwa uchache na Wajerumani, RB Leipzig.

Kwenye Kundi B, Mabingwa wa Hispania, Atletico Madrid ambao safu yao ya fowadi kutakuwa na wakali Luis Suarez na Griezmann watakuwa nyumbani Wanda Metropolitano kukipiga na FC Porto, wakati Jurgen Klopp na wakati wake Mohamed Salah na Sadio Mane watakuwa Anfield wakati chama lao la Liverpool watakapoikaribisha AC Milan ya Zlatan Ibrahimovic.

Kiboko ya makipa Ulaya, Erling Haaland na Borussia Dortmund yake ataanzia ugenini kwenye mchakamchaka wake wa kutetea Kiatu cha Dhahabu cha Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati watakapocheza na Besiktas, huku Sporting Lisbon itakuwa nyumbani kucheza na Wadachi, Ajax Amsterdam.

Mechi nyingine za kesho kwenye usiku huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, FC Sheriff watakuwa na kasheshe la kuwakabili Shakhtar Donetsk, huku mabingwa wa soka wa Italia, Inter Milan watakuwa na shughuli nzito ya kumkabili Karim Benzema na jeshi lake la Real Madrid kwenye mchakamchaka huo huko uwanjani San Siro. Macho ya wengi yanasubiri kuona kile ambacho masupastaa hao watafanya kuzisaidia timu zao hatua ya makundi ya michuano hiyo.