Waziri Ababu awavutia waya FIFA

WAZIRI mpya wa Michezo wakili msomi, Ababu Namwamba, amewavutia waya mabosi wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kwa lengo la kuokoa soka la Kenya.

Namwamba aliapishwa Alhamisi wiki iliyopita na kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Balozi Amina Mohammed siku iliyofuata.

“Kwenye siku yangu ya kwanza ofisini, niliwapigia simu FIFA ili kuanzisha mchakato wa kutatua mzozo uliopo, uliotupelekea kupigwa marufuku ya kushiriki mechi za kimataifa. Ni mazungumzo ya awali na niliwahamisha kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao kupata suluhu ili marufuku hiyo iondolewe,” anasema Namwamba.

FIFA ilifungia Kenya Februari mwaka huu baada ya Balozi Amina kuivunja ofisi ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kwa madai ya ufisadi na ubadhirifu wa mali za shirikisho na kwenye nafasi hiyo, akateua Kamati Shikilizi kuongoza soka nchini ambayo muhula wake ulimalizika mwezi uliyopita.

Kwenye kufikia uamuzi huo, FIFA iliamrisha Serikali ya Kenya iirejeshe viongozi wa FKF na pia kufungua Kandanda House ambayo ipo ofisi za FKF, hata hivyo amri hizo hazikutimizwa.

Na huku FIFA ikitarajiwa kuendelea kushikilia msimamo huo, Namwamba kwa upande wake anasema, anachokusuduia ni kuhakikisha suluhu inapatikana kwa kuzingatia sheria.

“Malengo ni kupata suluhu kwenye soka letu kwa kuzingatia sheria na matamanio ya umma. Waziri Amina alishanifafanulia jinsi mambo yalivyo na langu ni kusisitiza kuwa ni lazima tuzingatie sheria la sivyo, malumbano ya uongozi yataendelea. Ni lazima tunyooshe hilo,” alisisitiza Waziri wa Vijana, Michezo na Sanaa.