Watatu wakimbia kushuka daraja Zambia

WACHEZAJI watatu Wakenya wameanza kufunganya virago tayari kujitoa kwenye klabu zao zilizoshushwa daraja kwenye ligi kuu ya Zambia.
Kiungo wa timu ya taifa ya chipukizi Rising Stars, Teddy Osok tayari kadhibitisha kuwa anaondoka katika klabu yake ya Kitwe United iliyoteremshwa daraja wiki tatu zilizopita.

Kitwe ndio wamevuta mkia kwenye ligi hiyo msimu huu wakiwa na ushindi wa mechi tatu pekee, na vipigo 19 pamoja na sare 11 huku ligi hiyo ikiwa imesalia na raundi moja kufika tamati


"Mkataba wangu nao unafika kikomo na mechi ya  mwisho ya ligi kisha nitarejea nyumbani. Kwa sasa sitaki kuzungumzia mahesabu yangu ya siku za usoni. Nahitaji kupumzika kwanza kabla ya kujua nini cha kufanya," Osok kasema.


Osok alijiunga na Kitwe Oktoba 2020 baada ya kuikacha Wazito FC na kwa mkataba wa mwaka mmoja. Baada ya kuchujwa, Kitwe imeanza mikakati ya kuwaondoa wachezaji wake wa kigeni ila Osok alikuwa tayari ameshafanya uamuzi wa kujichuja.
Vile vile kule Napsa Stars ambako wanacheza kipa Shaban Odhoji na fulu beki David 'Calabar' Owino, nao wanapanga kujichuja baada ya klabu yao kuchujwa  pia kwenye ligi.


Owino anaripotiwa kuwindwa na klabu kadhaa za huko huko Zambia zilizosalia kwenye ligi kuu hasa kutokana na CV yake nzuri ya miaka mitano alipoichezea Zesco United kabla ya kujiunga na Napsa mwanzoni mwa msimu huu. Odhoji naye anatoka ila bado hajasema atakakokwenda.Ligi ya Zambia inafika kikomo rasmi Jumapili hii.