Sharks, Rangers nani kivuruge?

UBINGWA Ligi Kuu Kenya upo mikononi mwa Tusker FC kupoteza licha ya kufungamana kwa pointi na Kakamega Homeboyz.

Kinachowafanya Tusker FC kuwa kileleni mwa msimamo wa FKFPL ni uwiano mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ila wanafahamu fika bado ni mapema kuanza kusherehekea.

Hilo alilidhibitisha mwenyewe kocha wa Tusker FC, Robert Matano, baada ya ushindi mgumu dhidi ya Bidco United mwishoni mwa wiki iliyopita.

Matano alisema ligi bado haijaisha na ubingwa upo wazi wakiwa wamebakisha mechi moja kuhitimisha msimu wa 2021/22.

Naye kocha wa Homeboyz, Bernard Mwalala, bado anaamini lolote linaweza kutokea katika mechi za mwisho wa msimu akisisitiza umuhimu wa wao kushinda tena kwa idadi kubwa ya mabao endapo mambo watawaendea kinyume wapinzani wao.

Homeboyz wamezidiwa mabao manne na Tusker FC na Mwalala amekereka na Talanta FC kutotokea uwanjani mechi ya mwishoni mwa wiki iliyopita akisema imewanyima fursa kuwakaribia zaidi Wanamvinyo.

“Tusker wanajivunia uwiano mzuri wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa hivyo mapambano ndani ya uwanja dhidi ya Talanta ingetupatia nafasi kuwasongelea kwani nilikua nina imani wachezaji wangu wangefunga mabao mengi kutokana na maandalizi tuliyokua nayo,” alisema Mwalala.

Waliyosimama kati ya ama Tusker FC au Homeboyz kuwa mabingwa ni Posta Rangers na Kariobangi Sharks. Tusker FC watakua kwenye uwanja wao wa nyumbani kuwakaribisha Rangers huku Homeboyz wakiwa nyumbani dhidi ya Sharks.

Tusker FC walipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Rangers bao la pekee likifungwa na Bernard Ondiek lakini Matano ana rekodi nzuri katika mechi tano za mwisho akishinda tatu na kutoa sare mbili.

Homeboyz nao walishinda mechi ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Sharks kwa bao lililofungwa kwa njia ya penalti na David Okoth ila katika mechi tano za mwisho vijana wa Mwalala wameshinda mechi mbili, kupoteza mbili na kutoa sare mechi moja.

Katika mechi za kufunga pazia FKFPL wikendi hii, Tusker FC na Homeboyz kila moja atataka kushinda mechi yake huku wakiwa na matumaini mpinzani wake hatachukua pointi na kwamba atavurugiwa sherehe.