OKERE YUKO TAYARI STARLETS

Thursday April 22 2021
star pic
By John Kimwere

KOCHA mpya wa timu ya taifa ya wanawake ya Harambee Starlets, Charles Okere anasema yuko tayari kwa kibarua cha kuongoza kikosi hicho.

Okere alitwaa wadhifa huo wiki iliyopita  baada ya kocha, David Ouma kupigwa kalamu na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF). Okere atasaidiana na Godfrey Oduor na Mildred Cheche waliokuwa makocha wasaidizi katika timu ya KCB ya Ligi Kuu ya Betking Kenya Premier (BKPL).

''Bila shaka ni heshimu kubwa kuteuliwa kwa wadhifa wowote katika timu ya taifa. Ninafahamu wazi ni mtihani mgumu lakini nipo tayari kuonesha ujuzi wangu,'' alisema na kuongeza kuwa analenga kusaidia vigoli wa taifa kushinda mataji mbali mbali kwenye mechi za kimataifa.

Aidha anasema yupo tayari kufanya kazi ya kunoa kikosi hicho kwa dhati. Okere anashukuru vinara wa FKF kwa kutambua uwezo wake na kumtwika jukumu la kunoa kikosi hicho kuelekea kibarua kilicho mbele yao.

Starlets itashiriki mechi za kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Afrika katika soka la wanawake (AWCON) na itakuwa ikilenga kushiriki kwa ngarambe hiyo itakayofanyika nchini Morocco mwaka ujao.

Okere aliteuliwa kusaidiana na kocha, Robert Matano kunoa Tusker FC ambapo wameisadia kutwaa uongozi wa mapema kwenye kampeni za ligi kuu.  Tusker FC inaongoza katika jedwali la kipute hicho kwa kuzoa alama 36, sita mbele ya KCB.

Advertisement
Advertisement