Nyota Starlets anukia kutua Morocco

Monday August 01 2022
moroco pic
By RUTH AREGE

STRAIKA wa Harambee Starlets, Violet Wanyonyi Nanjala, itamulazimu kusubiria hadi Agosti 20 mwaka huu kukamilisha uhamisho wa kujiunga na timu ya wanawake ya Morocco, Club de Municipal, inayoshiriki daraja la pili nchini Morocco.

Mchezaji huyo wa zamani wa Trans Nzoia Falcons ya Ligi Kuu ya Wanawake, aliisaidia timu yake kusalia kwenye ligi msimu uliopita, Falcons ikishika nafasi ya saba na pointi 27.

Akizungumza na MWANASPOTI kwa njia ya simu, Wanyonyi amesema swala la kujiunga na Club de Municipal ni jambo ambalo hana uhuru wa kuzungumzia.

“Swala hiyo siwezi kulizungumzia kwasasa, nasubiria maelewano ya pande zote mbili. Nikifanikiwa kuenda habari hiyo nitaiweka wazi,” alisema straika huyo.

Wanyonyi alifanya majaribio na timu hiyo Machi mwaka huu na kuushawishi uongozi wa klabu hiyo kusaka saini yake.

Winga huyo ambaye aliwahi kukipiga Vihiga Queens kwa mkopo, alifanikiwa kufunga mabao manne wakati wa mashindano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) yaliyofanyika Septemba mwaka jana jijini Nairobi.

Advertisement

Nyota yake iling’aa zaidi alipofunga moja kati ya mabao mawili Vihiga Queens ilipocheza na ASFAR ya Morocco Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.


Advertisement