Mwendwa kuchunguzwa FIFA

WANASEMAGA siku ya kufa nyani, miti yote huteleza. Sasa sikia, mbunge limemwita Rais wa Shirikisho la soka nchini FKF, bwana Nick Mwendwa kujibu madai ya ufisadi huku nayo FIFA ikimtoka.
Kwa kawaida Shirikisho hilo la soka duniani huchukulia hatua kali taifa  pale serikali yake inapoingilia utendaji wa mwanachama wake.
Lakini raundi hii baada ya Mwendwa kukutwa na sakata la ubadhirifu wa Sh11 milioni, FIFA imetoa baraka zake kwa jamaa kuchunguzwa na serikali.
Kamati ya Uhasibu wa fedha za umma bungeni (PAC) tayari imemwita Mwendwa kwenye kikao ambacho anapaswa kufafanua ni jinsi gani alivyoweza kufaidi Sh11 milioni kama marupurupu kutoka kwa akaunti ya Shirikisho.
"Itakuwa vyema kwa kamati hii kusikia kutoka kwake Bwana Mwendwa kuhusu alikozipeleka fedha hizo na kwa nini alizuchukua pasi na kufuata utaratibu unaotakiwa." amesema mwenyekiti wa kamati hiyo Opiyo Wandayi ambaye ni mbunge wa Ugunja.
Lakini ngoma haiishi hapo. Afisi ya mwongoza mashtaka nchini DCI  nayo pia imezivamia afisi za FKF kuchunguza madai mengine ya ufisadi inayohusiana na Sh245 milioni iliyotolewa na serikali kama bajeti ya kuisapoti timu ya taifa Harambee Stars wakati wa AFCON 2019.
Mwendwa na afisi yake wanashtumiwa kwa kuwa na matumizi mabaya ya fedha hizo huku kiasi kikubwa kikiishia mifukoni mwa maafisa wa FKF akiwemo Rais huyo.
Afisi ya Msajili wa fani za Michezo nchini vile vile inakusudia kufanya ukaguzi wa vitabu vya kifedha vya FKF baada ya Waziri wa Michezo Balozi Amina Mohammed kutoa amri hiyo Oktoba 15.
Amri hiyo ilitolewa na Amina siku moja tu baada ya ombi la Mwendwa kwenye mahakama Kuu kutupiliwa mbali.
Kwenye ombi lake hilo, Mwendwa aliitaka  Mahakama Kuu kuizuia afisi ya DCI dhidi ya kumchunguza na kumkamata kwa madai ya ubadhirifu wa fedha za Shirikisho.
Kulingana na Katibu wa Kudumu katika Wizara ya fedha, Joe Okudo afisi ya DCI ilizivamia afisi ya FKF kuanza uchunguzi wa kina ikiwa ni baada ya kupokea baraka  kutoka kwa FIFA.
"Tumekuwa tukizungumza na FIFA na tuliweza kufanikiwa kuwashawishi kwenye madai dhidi ya FKF. Kwa baraka zao wameturuhusu kuingilia kati suala la usimamizi wa FKF ili tuweze kusafisha uovu unaoendelea." Okudo kadhibitisha.
Moja kati ya ishu inayochunguzwa sana ni suala la FKF kutumia ujanja na kufanikiwa kupata bajeti maradufu ya kuiandaa Harambee Stars wakati wa dimba la AFCON 2019. Okudo anasema kando na bajeti ya Sh245 milioni iliyotolewa na serikali, FKF ilifanikiwa kuishawishi FIFA kuiongezea fedha zingine kibao.
Kwa mujibu wa vitabu vya ukaguzi, Sh57  milioni kati ya Sh245 milioni iliyotolewa na serikali, zilitoweka katika njia isiyoeleweka.
"Stakabadhi za beki na pia vitabu vya kifedha havikutolewa kwa mhasibu wa serikali kudhibitisha kiasi haswa kilichotumwa kwenye akaunti mbalimbali za benki za wachezaji na benchi la ukufunzi ambao FKF inadai ilitumia fedha hizo kuwalipa." Okludo kaongeza.
Okudo amesisitiza kuwa safari hii Mwendwa hana pa kujificha baada ya FIFA kuipa serikali ruhusa kuichunguza FKF.