Mwenda amchimba mkwara Uchebe Kenya

Tuesday August 10 2021
mwenda pic
By Eliya Solomon

IKIWA imesalia mizunguko mitatu kabla ya msimu huu wa Ligi Kuu Kenya ‘KPL’ kutamatika, Mtanzania anayeichezea KCB, Ramadhan Mwenda amemtangazia vita aliyekuwa kocha wa zamani wa Simba, Patrick Aussems ‘Uchebe’ ambaye kwa sasa anainoa AFC Leopards SC.

KCB ni miongoni mwa klabu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa KPL, kabla ya mchezo wao wa jana, Jumapili dhidi ya Gor Mahia, walikuwa wakiongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 57 huku wakifuatiwa na Tusker iliyokuwa nafasi ya pili ikiwa na pointi 55.

Katika mizunguko hiyo mitatu iliyobakia kwa kila timu, KCB wanaonekana kuwa na ratiba ngumu kwa kutakiwa kukabiliana na Vihiga United, AFC Leopards SC na City Stars.

Beki huyo wa kimataifa wa Tanzania ambaye katika mzunguko wa 30 wa KPL alikuwa sehemu ya kikosi bora cha wiki, alisema kwa sasa kila mchezo ambao upo mbele yao ni fainali na mpango wao ni kuvuna pointi kwenye kila mchezo ili watimize ndoto zao za kutwaa ubingwa.

“Zimebaki mechi tatu tu ambazo tunatakiwa kuweka mkazo ili tuchukue ubingwa katika mazingira kama haya ukiteleza kidogo unaweza kujituka ukiondoka kwenye mstari, kila mchezo kwetu unauzito mkubwa sana, hakuna timu ambayo tunaihofia lakini tunaziheshimu.”

Haikuwa kazi nyepesi, msimu ulikuwa mgumu na changamoto zilikuwa nyingi lakini jambo zuri ni kwamba kama timu tumekuwa pamoja tulipopoteza tulipoteza wote na tuliposhinda tulifurahi pamoja, naamini tunaweza kutwaa ubingwa,” alisema beki huyo.

Advertisement

Mwenda amekuwa na wakati mzuri akiwa na KCB huku akitumika kama beki wa kati sambamba na Nashon Nanyendo wawili hao wakishirikiana na wenzao kwenye ukuta wa timu hiyo, wamelifanya chama lao kuruhusu mabao machache zaidi kwenye ligi hiyo.

KCB imeruhusu nyavu zake kuguswa mara 20 kabla ya mchezo wa jana huku wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Tusker wakifungwa mabao 24 na Nairobi City yakiwa 23.

Wakati KCB ikiwa na kibarua kizito mbele ya Vihiga United, AFC Leopards SC na City Stars, wapinzani wao wakuu kwenye mbio za ubingwa, Tusker wao michezo yao iliyopo mbele yao ni dhidi ya Homeboyz, Nzoia Sugar na Bidco United.

Advertisement