Masaibu ya Kakamega Homeboyz, Mwalala abadilisha Kiswahili

WANASEMA mbaazi ishindwapo kuzaa, husingizia jua. Ndicho unachoweza kusema anakifanya kwa sasa kocha wa Kakamega Homeboyz, Bernard Mwalala baada ya kikosi chake kupoteza fursa adimu ya kushinda kombe la ligi kuu msimu huu.
Ingawaje Homeboyz bado wanayo fursa ya kutwaa kombe lao la kwanza la ligi kuu msimu huu, fursa hiyo ni ndogo mno ikilinganishwa na hali ilivyokuwa wiki tano, sita zilizopita.
Homeboyz waliongoza msimamo wa jedwali toka  mzunguko wa kwanza hadi wiki mbili zilizopita walipobanduliwa kileleni na mabingwa watetezi Tusker FC.
Wakati mmoja Homeboyz walikuwa wamefungua gepu la pointi 12 kati yao na Tusker ila sasa wanatoshana alama 57 zikiwa zimesalia mechi mbili.
"Ndio kuna kipiundi tulikuwa tumefungua pengo la alama 12 na sijui nini kilichotokea. Ila vitu hivi hutokea kwenye soka sio tu kwa Homeboyz. Kote duniani hivi vitu hutokea," Mwalala alisema juzi kati akisisitiza bado wapo kwenye kinyang'anyiro.
Hata hivyo Tusker wamesalia kileleni kwa tofauti ya magoli. Homeboyz walipoteza uongozi huo kufuatia kuporomoka kwa fomu yao nzuri ya muda mrefu. Wikendi walikuwa na fursa ya kufungua tena mwanya huo walipochuana na AFC Leopards kwenye mechi yao ya kiporo lakini wakaishia kufinywa magoli 2-0 na hivyo kuwapa Tusker matumaini ya kutetea kombe lao.
Kwa msururu wa matokeo ya kufedhehesha kwenye mechi zao za hivi karibuni zilizochangia wao kupoteza uongozi, kocha Mwalala ameishi kudai kuwa ni uchovu wa msimu ndio umewalemea vijana wake na hivyo kuathiri makali yao uwanjani.
Lakini sasa Mwalala amebadilisha kiswahili na anasema kuwa kuna mambo mengine yaliyopelekea kupotea kwa fomu yao.
"Kama kocha kuna mambo ninayoyajua yanaendelea nyuma ya pazia yaliyotuathiri na kutupotezea kasi tuliyokuwa nayo. Hizi ni baadhi ya changamoto ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo na nisingelipenda kuzizungumzia. Mwisho wa siku la muhimu ni kwa kila mdau wa timu kuhakikisha anatekeleza wajibu wake jinsi inavyotakiwa," anasema.
Lakini haiishi hapo, Mwalala pia ameirushia lawama benchi lake akilitaja kuwa hafifu sana, jambo ambalo hakuwahi kulilalamikia timu ilipokuwa ikifanya vizuri hapo awali.
"Wachezaji wetu kwenye benchi hawajakuwa wenye msaada kwa timu kila tufanyapo mabadiliko kwa lengo la kubadilisha mkondo wa mechi. Ila hilo sio ishu kubwa linalochangia fomu yetu kushuka," ameongeza.