Leopards yatangaza vita kwa wapinzani FKF PL

Saturday May 29 2021
LEOPARDS PIC

Klabu ya AFC Leopards imetangaza hali ya hatari kwa wapinzani wao kwenye ligi kuu ya Betking hii ni baada ya kuwakomoa mabingwa wa zamani Mathare United 1-0 uwanjani Ruaraka.
Ushindi huo umempa ujeuri kocha wao mbelgiji Patrick Aussems anayesema timu hiyo kongwe Kenya inazidi kuimarika katika kila idara msimu huu chini ya uongozi wake.
Baada ya kushuka uwanjani mara 17,Ingwe ipo katika nafasi ya pili kwa jumla ya pointi 36,alama sawa na viongozi KCB wanaojivunia idadi nzuri ya mabao.
“Cha msingi kwetu tumepata ushindi,hata kama ni ushindi wa bao moja bado unasalia ushindi.Hata tungeshinda kwa idadi ya mabao matano kwa bila alama zingesalia zile zile tatu.Najivunia kwa kazi walioifanya wachezaji wangu japo ndio tulikuwa na nafasi ya kufunga magoli zaidi”,Ausseme amesema baada ya mechi ya kiporo ddhidi ya Mathare United.
Hata hivyo,Ingwe imepata pigo la kadi nyekundu katika mechi mbili mfululizo hii ni baada ya kiungo Collins Sichenje kutimuliwa uwanjani dakika za lala salama za ngarambe hiyo ya dhidi ya Mathare kwa kucheza ngware.
Naibu nahodha Isaac Kipyegon naye pia anatumikia marufuku ya mechi mbili kwa kulishwa kadi nyekundu katika mchezo wa sare tasa dhidi ya Posta Rangers.
Itakumbukwa kwamba nahodha Robinson Kamura naye alikosa mechi dhidi ya Nzoia Sugar na Vihiga United mtawalia kwa kosa hilo hilo la kuonyeshwa kadi nyekundu katika ushindi wao wa 1-0 ldhidi ya Nairobi City Stars Machi 6 ugani Kasarani.
“Leo pia tumepata kadi nyekundu kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita.Hii ina maana tutakuwa bila nguvu za wachezaji hao wawili muhimu katika mchezo ujao.Hata hivyo nina imani na wachezaji wangu wote na nitawahitaji tena kama kundi katika mechi zijazo dhidi ya Bidco na Posta Rangers.
“Kwa kweli tunazidi kuimarika mchezo baada ya mchezo.Tunapiga hatua muhimu kila siku katika jaribio la kuafikia malengo.Hilo kwangu ndio la umuhimu katika timu hiyo”.
Baadhi ya mashabiki wa AFC Leopards wanamuona Aussems kama mwalimu faafu atakaye ondoa nuksi ya ukame wa ligi wa kipindi cha miaka 22.
Jumapili,miamba hao wa soka Kenya watarejea tena mawindoni dhidi ya Bidco United uwanjani Ruaraka ikiwa ni mechi ya ligi kuu.


Imeandikwa na Vincent Voiyoh

Advertisement