KIPKURUI AFICHUA MAKUBWA YA GOR

Tuesday March 30 2021
kipru pic
By Thomas Matiko

STRAIKA mpya wa Nairobi City Stars, Nicholas Kipkurui kadai kuwa maisha magumu katika klabu ya Gor Mahia, yalitishia kuisambaratisha taaluma yake ya soka.
Kipkurui aliyejiunga na City Stars wiki tatu zilizopita baada ya kuvunja mkataba wake wa miaka mitatu na Gor anasema kuwa, msoto unaendelea Gor ulikuwa umeanza kuathiri kiwango chake cha mchezo.
Kule Gor imekuwa jambo la kawaida kwa wachezaji kucheleweshewa mishahara yao kwa hata zaidi ya miezi mitatu.
Ishu hiyo ndio Kipkurui anasema ilimfanya morali yake ya kucheza ishuke na katika hilo kuanza kuathiri uwezo wake wa kujifua na kujituma uwanjani.
“Unapoondoka nyumbani ukiwa na mawazo, hautaweza kujituma uwanjani kwa asilimia 100%. Kama mchezaji anayezingatia soka kitaaluma, ni lazima muda wote uwe mtulivu wa kimawazo na afya nzuri ndiposa utaweza kujituma inavyotakiwa uwanjani na mazoezini. Pale Gor hilo halingewezekana.” Kipkurui kakiri.
Kwake yeye uamuzi wa kuondoka Gor ulikuwa mwafaka kwa sababu kama angeendelea kuwa pale basi mambo yangeisha kumharibikia hata vibaya zaidi.
Kipkurui anasema kipindi akiwa Gor, mara si moja alifungiwa nyumba yake Nairobi kwa kushindwa kulipa kodi kwa wakati jambo lililomlazimu kurudi nyumbani kwao Kericho.
Matatizo yalipozidi, akaamua kuvunja mkataba kwa mujibu wa sheria za FIFA zinazomkubalia mchezaji kuitema klabu pale inaposhindwa kumlipa mishahara wake kwa miezi mitatu mfululizo. Kipkurui alijiunga na Gor 2017 baada ya kung’aa msimu huo akiichezea Zoo Kericho na kuisaidia kueupuka kushusha daraja kwa kufunga magoli 10. Akiwa Gor, aliishia kuwa mkombozi wa klabu akifanya mazoea ya kufunga mabao muhimu kwenye mechi kadhaa ambazo Kogalo walionekana kuhangaikia ushindi au kuepuka kipigo.


Advertisement