KAHATA AITISHA DOO MOB, GOR WAMCHOREA GIZA

TANGU aachiliwe na Simba SC Juni mwaka huu baada ya mkataba wake kumalizika huku kiwango chake kikishuka, kiungo Francis Kahata hajafanikiwa kupata klabu.
Baada ya kurejea nchini, kiungo ambaye hata kwenye timu ya taifa Harambee Stars tayari ameshatemwa, amekuwa akifanya mazoezi na Gor Mahia aliowachezea hadi 2019 kabla ya kwenda Tanzania.
Gor ambao wamekuwa na kipindi kigumu cha fedha msimu huu, walikuwa na nia ya kumsajili tena Kahata kwa ajili ya msimu ujao.
Uongozi wa Gor ulitegemea kuwa ungempata  Kahata kiurahisi lakini sasa umelazimika kuacha kumfukuzia kwa madai kuwa jamaa kawaitisha fedha nyingi kama malipo ya Sign on Fee (Fedha anazolipwa mchezaji huru kwa kukubali kujiunga na klabu).
"Ikiwa una bajeti ya Sh10 milioni na una mpango wa kusajili wachezaji saba ila mchezaji mmoja kati ya hao saba , kakuitisha kiasi chote hicho kama sign-on fee, je utaweza kuendelea na nia ya kumsajili? Mkurungezi wa Gor Lordvic Aduda kahoji.
Kwa sababu hiyo, uongozi umefanya maamuzi ya kuachana na kiungo wao huyo wa zamani na badala yake kuangalia kwingine.
"Hatuna fedha za kusajili wachezaji na ndio sababu tumeachana naye. Klabu zinahangaika na sio Gor tu hata Kariobangi Sharks inayomilikiwa na Rais wa Shirikisho Nick Mwendwa, mumeshuhudia wachezaji wakiondoka kwa wingi. Kwa hiyo kwa kile kiasi kidogo cha fedhxa tulichonacho, tutasajili wachezaji tutakaoafikiana nao." Aduda kaongeza.
Kwa sasa Gor wanaendelea kuwafukuzia mastraika watatu wa kigenin baada ya kuondoka kwa Mburundi Jules Ulimwengu na Tito Okello wa Sudan Kusini.
Kocha Mwingereza Mark Harisson kasema mpango alionao ni kujaza nafasi za mastraika hao wawili kwa kuwasajili watatu wa kigeni.
"Wapo mastraika watatu kutoka Nigeria, Malawi na DRC ninaohitaji. Msimu ujao tutakuwa na mastraika wa kigeni kwenye mchakato nilionao wa kukisuka kikosi kipya." Harisson kasema.