GHOST AIMALIZA CAREER YA WANYAMA HARAMBEE STARS

Tuesday September 07 2021
matiko pic
By Thomas Matiko

KAMA  kiungo Victor Mugubi Wanyama angali na matumaini ya kuichezea tena timu ya taifa Harambee Stars, basi aombe dua kocha Jacob Ghost Mulee aondoke.
Hii ni kwa sababu  sasa Ghost kakata kauli na kutangaza kwamba hana nia wala mipango ya kumtumia Wanyama akisisitiza kuwa muda wake Stars umekwisha.
Toka alipoteuliwa kwa mara ya tatu kuwa kocha wa Stars, Oktoba 2020, Ghost hajawahi kumwita hata mara moja kikosini Wanyama.
Mara kadhaa amekuwa akijitahidi kukwepa maswali kuhusu ni kwa nini hamwiti kikosini Wanyama aliyekuwa ni nahodha wa timu hiyo.
Lakini baada ya kuchoka kucheza kalongo-longo hiyo, Ghost kamaliza utata kwa kukata kauli na kusema kuwa hamhitaji kabisa Wanyama.
"Nilipoichukua timu (kutoka kwa Francis Kimanzi), tukiwa tunajiandaa kuchuana dhidi ya Comoros na Togo, sikumkuta Wanyama kwenye kikosi nilichoridhi. Ndicho kipindi nilichoamua lazima kuwe na mabadiliko na nikamteua Olunga kuwa nahodha mpya wa timu." Mulee kakata kauli.
Hii sasa ina maana kuwa career ya Wanyama na Stars huenda ikawa imefikia kikomo na ikiwa ana matumaini ya kuvalia jezi za taifa tena, basi itakuwa ni chini ya kocha tofauti ambaye anamhusudu.
Odada amtoa Wanyama Game
Lakini hata ikitokea akaja kocha mwingine, itakuwa vigumu sana Wanyama kuiwahi nafasi yake tena hasa baada ya mrithi wake kupatikana akiwa ni mchezaji chipukizi Richard Odada.
Odada anayecheza soka lake la kulipwa kule Serbia,  alipangwa kwenye  mechi yake ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Uganda Cranes na kuonyesha kiwango kikubwa kilichowafurahisha mashabiki na wachanganuzi wengi. Hii ni licha ya mechi hiyo kuishia kwa sare tasa.
Ghost alimpa mechi yake ya pili ya kitaifa dhidi ya Rwanda juzi Jumapili iliyomalizika kwa sare nyingine ya 1-1.
Bado tu dogo huyo wa miaka 21, alitisha akicheza kama kiungo mkabaji nafasi aliyokuwa akicheza Wanyama.
"Nafikiri chipukizi Odada kaonyesha kiwango kizuri katika mechi hizi na ukiniuliza mimi,  tatizo  tulilokuwa nalo la kiungo beki, sasa  tumelitatua. Kwa muda mrefu sijawahi kuona kiungo mkabaji kama Odada hapa Afrika. Alidhibiti safu ya kati kisawaswa, alitoa pasi za umakini zilizomfikia mlengwa na stamina yake ni ya ajabu. Hatuna tatizo tena kwenye safu ya kati." Ghost kasisitiza.
Wanyama aliyeichezea Stars mechi 60, alikabidhiwa unahodha wa Stars na kocha Mbelgiji Adel Amrouche akiridhi mikoba ya straika mstaafu Dennis Oliech.

Advertisement