BANDARI WAHAMIA NAIROBI

Friday September 17 2021
nai pic
By Sinda Matiko

KLABU ya Bandari FC imehamia mjini Nairobi ambapo itakuwepo kwa kipindi cha wiki nzima kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Bandari waliomaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimu uliomalizika mwezi uliopita, kwa sasa wamekita kambi katika uwanja wa Vapor Sports Ground, kule Ngong.
Watakuwa huko kwa  kambi ya siku sita na katika kipindi hicho, wanatarajia kushiriki mechi mbili za kirafiki.
"Tuliwasili Nairobi Jumatatu na tutaondoka Jumapili kurudi zetu Mombasa. Lengo la kudunga kambi Nairobi ni kwa sababu tuliona uhitaji wa kubadilisha hali ya hewa. Isitoshe mechi zetu nyingi za ugenini zipo nje ya Mombasa hivyo huu ni mchakato wa kuzoesha miili yetu hali tofauti ya anga na ile ya Mombasa."kasema afisa mawasiliano wa Bandari Steven  Heywood.
Mechi hizo mbili za kirafiki wanazojipangia zitakuwa dhidi ya timu zinazoshiriki ligi kuu msimu ujao.
"Mechi hizo ni kwa ajili ya kutesti viwango vyetu ya fitinesi kabla ya mwanzo wa ligi." kaongeza Mkurugenzi wa kiufundi Twahir Muhindi ambaye pia ni naibu kocha wa Harambee Stars.
Kando na hilo Muhiddin anasema Bandari wapo kwenye mchakato wa kuboresha kikosi chao kwa sajili wapya ila kwa sasa hawana mipango ya kuwaweka wazi.
Muhiddin kasisitiza kuwa kuna uhitaji mkubwa wa kukiboresha kikosi chao kwa sababu malengo waliyonayo kwenye msimu mpya ni kuboresha matokeo yao yaliyopita kwenye ligi kuu.
"Lengo letu kubwa kwa sasa ni kufanya vyema zaidi ya tulivyofanya msimu uliomalizika hivi majuzi na ndio sababu tunapanga kufanya pia na usajili ili kukirutubisha kikosi chetu.
Wiki iliyopita, Bandari iliwatema wachezaji watano na tayari imemsajili beki wa kati Rogers Aloro aliyeachiliwa na Tusker. Aidha inaendelea kuwafuatilia kiungo Faraj Ominde na strika  Chris Ochieng wote wakiwa wameachiliwa na Tusker.

Advertisement