AUSSEMS: SINA PRESHA

Thursday October 21 2021
ausems pic
By Sinda Matiko

"Sina presha mimi, presha ni ya bia na tairi la gari" Ndivyo alivyowahi kujichocha kocha wa AFC Leopards, Patrick Aussems msimu uliopita alipoteuliwa kuwa kocha wa klabu hiyo.
Lakini sasa Aussems kazidiwa na presha hiyo akiwa na hofu kubwa kuhusu uwezekano wa yeye kufanya usajili huku dirisha la usajili likikaribia kufungwa.
Hadi sasa Ingwe hawajasajili mchezaji hata mmoja kutokana na kile kikwazo walichowekewa na FIFA cha kutowaruhusu kufanya usajili wowote wa wachezaji wapya.
Kikwazo hicho waliwekewa baada ya kukosa kuwafidia makocha wao wawili wa zamani pamoja na wachezaji watatu waliowavunjiia mikataba yao bila ya kufuata utaratibu unaotakiwa.
Baya hata zaidi ni kuwa First 11 yote ya Ingwe iliondoka baada ya kumalizika kwa msimu uliopita. Kwa ujumla kocha Aussems aliwapoteza wachezaji 16 waliounda kikosi chake cha kwanza.
Na kutokana na marufuku hiyo, msimu huu Ingwe walilazimika kuwapandisha daraja hadi kikosi chao cha kwanza wachezaji wao wa timu ya chipukuzi.
Hii ndio timu ambayo kocha Aussems ameitumia kwenye mechi mbili za mwanzo wa msimu huu zmpya wa ligi kuu.
Walianza msimu kwa kuwalima mabingwa watetezi wa ligi kuu Tusker 1-0 kabla ya kushikwa sare tasa wikendi iliyopita na KCB, waliomaliza katika nafasi ya pili ligini msimu uliopita.
Licha ya kikosi hicho kuonyesha matumaini makubwa, kocha Aussems hana matumaini nacho sana kutokana na kuwa hakina uzoefu wa kutosha.
Ni kwa sababu hii ndio amekuwa akitamani kufanya usajili wa angalau wachezaji wazoefu ili kuweza kukirutubisha kikosi hicho.
"Kikosi chetu sio bora na sijui itakuaje sababu hatujaruhusiwa kusajili. Tumekuwa tukifanya kazi na kikosi kichanga mno kwa mwezi sasa. Licha ya hiyo tumefanikiwa kuanza vizuri lakini ninajua kuna wakati tutapata tabu kwa sababu tuna kikosi cha kubahatisha. Ni kikosi kichanga sana na kama hatutafanya usajili tutaumia." Aussems anahaha.
Hata hivyo mwanaspoti ina taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo kuwa uongozi wa Ingwe tayari imeafikiana na makocha Casa Mbungo na Marko Vesijevic kuhusu namna itakavyomalizana nao.
Pia imewasaka wachezaji Vincent habamahoro anayedai Sh1.8 milioni na Dickson Ambundo waliowashtaki vile vile kwa lengo la kufikia maagano nao kuhusu namna itakavyowafidia.
"Uongozi umeshazungumza na makocha hao na kufikia mapatano. Sasa ipo kwenye mazungumzo na wachezaji. Hao ndio wanaopaswa sasa kuwasiliana na FIFA kuifahamisha kuhusu maagano hayo kisha ndio marufuku iondolewe. Mategemeo yetu ni kuwa kikwazo kitaondolewa kufikia wiki ijayo ili tuweze kusajili." Amedokeza mmoja wa wanachama wa ngazi ya juu ya klabu.


Advertisement